Watuhumiwa saba wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Same leo, Februari 19, 2026, wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali yanayohusiana na dawa za kulevya aina ya mirungi, huku mmoja wao akiwekewa amri ya kuwa chini ya uangalizi wa Polisi kwa miaka mitatu.

Kwa mujibu wa taarifa za mahakama, kesi saba zimefunguliwa, kila moja ikiwa na mtuhumiwa mmoja. Watuhumiwa wote walisomewa mashtaka yao na walikana tuhuma zinazowakabili, na mashauri yao kupangiwa tarehe nyingine.

Katika kesi ya kwanza, Goodlak Bariki Mungulu anashtakiwa kwa kupatikana na mirungi yenye uzito wa kilo 1.8. Shtaka hilo liliwasilishwa na Wakili wa Serikali, Jackson Matowo, mbele ya Mheshimiwa Christanta Chitanda, Hakimu Mfawidhi. Mshtakiwa alikana shtaka hilo na shauri lake limepangwa kutajwa tena Juni 24, 2024. Ingawa shauri hilo lina dhamana, mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Kesi ya pili inamhusu Athuman Tuarira Kivuma, anayekabiliwa na shtaka la kusafirisha mirungi yenye uzito wa kilo 27. Shtaka liliwasilishwa na Wakili Matowo mbele ya Hakimu Chitanda. Mshtakiwa alikana na shauri lake limepangwa tena Juni 24, 2024.

Katika kesi ya tatu, Nuru Mbonea Mndeme anashtakiwa kwa kusafirisha mirungi kilo 25. Mashtaka yake yalisomwa mbele ya Hakimu Chitanda, naye alikana. Shauri lake limepangwa tena Februari 24, 2026.

Kesi tatu nyingine zilisikilizwa mbele ya Mheshimiwa Hellen Hozza, Hakimu Mkazi Mwandamizi. Katika mashauri hayo, Youze Eliwaha Kitua anakabiliwa na shtaka la kusafirisha mirungi kilo 34, Ahadi Mbazi Mnjama kilo 26 na Edson Elihazina Kibaja kilo 24. Mashtaka yao yalisomwa na Wakili wa Serikali Alex Rusibamayila, na wote walikana tuhuma hizo. Mashauri yao yamepangwa tena Machi 2, 2026; Machi 4, 2025; na Machi 3, 2026 mtawalia.

Kwa upande wa kesi ya saba, Mganga Wahidi Dorovu alipandishwa mahakamani kwa ajili ya kuwekewa chini ya uangalizi ya kuwa na tabia njema ya kutokufanya uhalifu wowote. Mahakama iliamuru awe chini ya uangalizi wa Polisi Same kwa kipindi cha miaka mitatu na kuripoti kituoni kila mwezi, kwa masharti ya kutojihusisha na uhalifu wowote, ikiwemo biashara au matumizi ya dawa za kulevya.

Hatua hiyo inaonyesha kuendelea kwa juhudi za vyombo vya dola katika kukabiliana na biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya katika Wilaya ya Same na maeneo jirani.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...