WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), ametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile.

Balozi Kombo ametoa wito huo Februari 13,2026 katika Kikao cha Ngazi ya Juu cha Bonde la Mto Nile kilichofanyika pembezoni mwa Mkutano Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia kuanzia February 11-15, 2026.

Kupitia kikao hicho Mheshimiwa Waziri Kombo alithibitisha dhamira ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha ushirikiano, mazungumzo na usimamizi endelevu wa rasilimali maji ya Mto Nile kwa manufaa ya nchi zote zinazozunguka bonde hilo.

Akizungumza mbele ya Mawaziri na wawakilishi kutoka nchi za Bonde la Nile, Waziri Kombo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya taasisi za bonde hilom na kusisitiza kuwa uimarishaji wa mifumo hiyo utatoa mfumo wa kudumu utakaoratibiwa vizuri na hivyo kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha matumizi ya haki na yenye uwiano ya rasilimali maji ya pamoja.

“Tunaikaribisha na kuiunga mkono kikamilifu kuanzishwa kwa Tume ya Bonde la Mto Nile,” alisema Waziri Kombo na kuongeza “Muhimu zaidi, tunaunga mkono juhudi zinazoendelea za kuzijumuisha nchi zote zinazohusika na kupitia mazungumzo ya kujenga na uelewano wa pamoja, tutaweza kutatua tofauti zetu.”

Waziri Kombo alieleza kuwa Tanzania inaunga mkono utekelezaji wa Mpango wa Uwekezaji wa Bonde la Mto Nile unaojumuisha miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha usalama wa maji, nishati, uzalishaji wa chakula na uhifadhi wa mazingira katika ukanda wa Bonde la Nile.

Alibainisha kuwa uwekezaji wa pamoja katika miundombinu, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na miradi ya nishati jadidifu utapunguza athari za changamoto zilizopo na kufungua fursa za ustawi wa pamoja kwa nchi wanachama.

Amezisihi nchi husika kuendelea na mazungumzo na kuepuka hatua zinazoweza kuongeza mvutano na kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuhimiza mazungumzo ya amani, kuheshimiana na kutafuta suluhisho za changamoto kwa misingi ya Kiafrika ili kulifanya Bonde la Nile kuwa mfano wa umoja na maendeleo endelevu barani Afrika.

Mkutano huo uliandaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Mheshimiwa Gedion Timotheos na kuhudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi za Bonde la Nile ambazo ni Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Ethiopia na Sudani kusini.

Tanzania Yazipongeza Ghana, Zimbabwe, Sierra Leone na APRM AFRIKA

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezipongeza Jamhuri za Ghana, Zimbabwe na Sierra Leone na Sekretarieti ya Mpango wa Kujitathmini kwa Hiari Afrika (APRM) kwa kukamilisha mchakato wa tathmini wa hiari chini ya utaratibu wa African Peer Review Mechanism (APRM) wa Umoja wa Afrika.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Februari 13, 2026 jijini Addis Ababa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipomwakilisha katika Kikao cha 35 cha Kawaida cha Jukwaa la Kujitathmini Barani Afrika la Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kilichofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kuanzia Februari 11–15 , 2026.

Mhe. Waziri Kombo amesema hatua iliyofikiwa na nchi hizo inaonesha dhamira ya kweli ya nchi hizo katika kuimarisha misingi ya utawala bora, uwajibikaji ili kufikia maendeleo endelevu barani Afrika.

Waziri Kombo pia amewasilisha pongezi za Tanzania kwa Sekretarieti ya APRM ya Umoja wa Afrika (AU) kwa kazi kubwa na ya kitaalamu inayoendelea kufanya katika kuratibu tathmini hizo pamoja na kusimamia utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa na nchi wanachama.

“Sekretarieti ya APRM ya AU imeendelea kuwa chombo muhimu katika kuhamasisha uwazi, uwajibikaji na kubadilishana uzoefu miongoni mwa nchi wanachama, Tanzania inaipongeza sana Sekretarieti,” alisema Waziri Kombo.

Waziri Kombo aliahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kikamilifu na Sekretarieti ya APRM pamoja na nchi nyingine za Afrika katika kutekeleza na kufanikisha malengo ya chombo hicho na kusisitiza kuwa kupitia mshikamano na ushirikiano wa dhati, mataifa ya Afrika yataweza kuimarisha taasisi zake, kukuza demokrasia na kuhakikisha kunakuwepo na maendeleo jumuishi kwa manufaa ya wananchi wake.

Kikao hicho cha ngazi ya juu kiliandaliwa chini ya Mpango wa Kujitathmini kwa Hiari Barani Afrika wa Umoja wa Afrika (AU) uliwakutanisha viongozi wa Afrika kwa lengo la kupitia maendeleo ya utawala bora, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji barani Afrika. Mkutano huo ulihudhuriwa na Marais kutoka nchi za Angola, Burundi, Namibia, Msumbiji, Zimbabwe, Makamu wa Rais wa Kwanza wa Uganda na Mawaziri wa Mambo ya Nje ambao waliwawakilisha Wakuu wa Nchi nyingine za Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo katika picha ya Pamoja na Baadhi ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika baada ya ufunguzi wa Kikao cha 35 cha Kawaida cha Jukwaa la Kujitathmini Barani Afrika la Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kilichofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kuanzia Februari 11–15 , 2026.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Mhe.Henry Oryem Okell wakati wa Kikao cha 35 cha Kawaida cha Jukwaa la Kujitathmini Barani Afrika la Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kilichofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kuanzia Februari 11–15 , 2026.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Mhe. Gedion Timotheos wakati wa Kikao cha Ngazi ya Juu cha Bonde la Mto Nile kilichohusisha Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka katika Nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile kilichofanyika February 13,2026 pembezoni mwa Mkutano Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia kuanzia February 11-15, 2026.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...