Manyoni, Singida, Februari 12, 2026 — Ziara ya mafunzo ya wataalamu wa Idara ya Misitu Zanzibar imeingia siku ya pili leo kwa ujumbe huo kuanza rasmi mafunzo ya vitendo katika Shamba Darasa la Nyuki la TFS, wilayani Manyoni.

Mafunzo hayo yameanza kwa mada ya uanzishaji na usimamizi bora wa Hifadhi za Nyuki (Bee Reserves) iliyowasilishwa na Askari wa Uhifadhi – Ufugaji Nyuki Wilaya ya Manyoni, Jacline Leshabari, akieleza hatua za kisheria, kiutawala na kiikolojia zinazohitajika katika kuanzisha na kulinda maeneo maalum ya nyuki.

Akiwasilisha mada hiyo, Leshabari amesema hifadhi za nyuki zimekuwa nyenzo muhimu si tu katika kuongeza uzalishaji wa asali na mazao yatokanayo na nyuki, bali pia katika kulinda misitu na bioanuai. “Usimamizi madhubuti wa hifadhi hizi unahakikisha upatikanaji endelevu wa malighafi za nyuki huku ukihifadhi mfumo wa ikolojia,” amesema.

Kwa mujibu wa ratiba ya mafunzo, wataalamu hao kutoka Zanzibar wanatarajiwa pia kujionea kwa vitendo utambuzi wa maeneo ya hifadhi, uwekaji wa mizinga ya kisasa, pamoja na mbinu za kushirikisha jamii katika kulinda na kunufaika na rasilimali za nyuki.

Mkurugenzi wa Idara ya Misitu Zanzibar, Said Juma Ali, amesema mafunzo ya siku ya pili yamewapa mwanga mpana juu ya namna TFS inavyounganisha uhifadhi na uchumi wa jamii kupitia sekta ya nyuki. Amesisitiza kuwa uzoefu huo utasaidia Zanzibar katika mpango wake wa kuanzisha hifadhi za nyuki na kuendeleza utalii wa nyuki.

Ziara hiyo ya siku tano inatarajiwa kuendelea kwa mafunzo zaidi kuhusu uchakataji wa asali, viwango vya ubora na masoko, huku ushirikiano kati ya TFS na Idara ya Misitu Zanzibar ukitajwa kuwa kichocheo cha mageuzi ya sekta ya nyuki nchini.




 

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...