Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) leo imepokea ujumbe wa wadau wa maendeleo kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Mastercard Foundation, Education for Sub-Saharan Africa (ESSA), Tanzania Education Network (TEN/MET), African Centre for School Leadership (ACSL), Teach United na Educate kwa ajili ya kujadili ushirikiano wa kuimarisha uongozi wa shule za sekondari nchini.

Akifungua kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid, alieleza kuwa taasisi hiyo ina dhamana ya kitaifa ya kuwa kitovu cha ubora katika mafunzo, utafiti na ushauri kuhusu uongozi, usimamizi, utawala wa elimu pamoja na uhakiki wa ubora wa elimu.

Alisema kwa miongo kadhaa ADEM imekuwa mkono wa kimkakati wa Serikali katika kujenga uwezo wa wasimamizi wa elimu kuanzia wakuu wa shule, waratibu wa elimu wa kata, hadi maafisa wa elimu wa wilaya, mikoa na ngazi ya taifa.

“ADEM haijikiti tu kwenye mafunzo bali pia inafanya tafiti za kitaaluma zinazosaidia kuunda sera za elimu, kutoa huduma za ushauri kwa shule na halmashauri pamoja na kuandaa mifumo na zana za kuboresha utendaji wa shule. Kupitia mtandao mpana wa taasisi na maafisa wa elimu katika Mamlaka zote za Serikali za Mitaa, ADEM ina uwezo wa kutekeleza programu kubwa za kuimarisha uongozi na usimamizi wa shule nchini,” alisema Dkt. Maulid.

Katika kikao hicho, ADEM iliwasilisha maeneo yake muhimu ya utaalamu ikiwemo uongozi na utawala wa elimu, upangaji wa sera na uhakiki wa ubora, mipango ya maboresho ya shule, ufundishaji unaozingatia usawa wa kijinsia, uongozi wa kitaaluma wa ufundishaji, maendeleo ya taaluma ya walimu, ushirikishwaji wa jamii katika usimamizi wa shule pamoja na ufuatiliaji na tathmini ya mipango ya kimkakati ya shule.

Majadiliano pia yalijikita katika utekelezaji wa programu ya LIT-LEAD, inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya ADEM na VVOB – Education for Development kwa ufadhili wa Mastercard Foundation.

Programu hiyo inalenga kuziba pengo la uongozi katika shule za sekondari nchini kwa kuwajengea uwezo wakuu wa shule katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji, kukuza uongozi jumuishi unaozingatia usawa wa kijinsia, kuimarisha mipango ya maboresho ya shule pamoja na kuboresha utawala wa shule kupitia ushiriki wa kamati za shule na wazazi.

Kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa programu hiyo, ADEM na VVOB zilifanya tathmini ya mahitaji ya mafunzo (Training Needs Assessment - TNA) iliyowahusisha viongozi wa shule, maafisa wa elimu wa wilaya pamoja na wawakilishi wa Wizara ili kuhakikisha maudhui ya mafunzo yanaendana na mazingira halisi ya elimu nchini Tanzania.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa VVOB nchini Tanzania, Bi. Sarish Hiribae, alipongeza ushirikiano uliopo kati ya VVOB na ADEM katika kuimarisha uongozi wa shule za sekondari nchini.

Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe wa wadau kutoka Mastercard Foundation, Bi. Tracy Osio, aliipongeza ADEM kwa ushirikiano wake na VVOB pamoja na wadau wengine, akieleza kuwa ushirikiano huo una uwezo mkubwa wa kuleta mageuzi katika uongozi wa elimu kupitia utekelezaji wa programu ya LIT-LEAD.

Katika majadiliano hayo, wadau pia waliuliza maswali kuhusu mifumo ya ADEM ya kuhakikisha ubora wa mafunzo yanayotolewa. Kujibu hilo, ADEM ilieleza kuwa ubora wa mafunzo huhakikishwa kupitia tathmini za mahitaji ya mafunzo, warsha za uthibitishaji wa maudhui pamoja na uhakiki wa ubora unaofanywa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa kozi za muda mrefu.

Aidha, Dkt. Lucas Mzelela alieleza kuwa ushirikiano kati ya ADEM na VVOB ulianza mwaka 2025 na unatarajiwa kudumu kwa kipindi cha miaka sita. Katika kipindi hicho, taasisi hizo zitashirikiana kujenga uwezo wa wakuu wa shule za sekondari katika uongozi bora na usimamizi madhubuti wa elimu.

Aliongeza kuwa ushirikiano huo pia utahusisha uandaaji wa moduli za mafunzo kupitia mfumo wa kidijitali wa Learning Management System (LMS) ili kuwafikia viongozi wengi zaidi wa elimu nchini.

Kupitia ushirikiano wa kimkakati kama programu ya LIT-LEAD, ADEM inaendelea kuwa mhimili muhimu katika kuendeleza ajenda ya taifa ya kuboresha elimu na kuimarisha uongozi wa shule kwa manufaa ya wanafunzi nchini.










Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...