Mbeya- Jumanne, Machi 31, 2026


Katika kuadhimisha miaka 25 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Kampasi ya Mbeya imefanya shughuli za kijamii, ikiwemo kutembelea na kutoa misaada kwa vituo viwili vya watoto yatima jijini Mbeya.

Shughuli hiyo imehusisha watumishi wa chuo hicho wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, pamoja na Mkurugenzi wa Kampasi ya Mbeya, Ndugu Saidy Nzagamba. Vituo vilivyotembelewa ni Kituo cha Watoto Yatima Iwambi kilichopo mtaa wa Iwambi na Kituo cha Bi Aisha Foundation kilichopo mtaa wa Soweto.

Katika ziara hiyo, TPSC Kampasi ya Mbeya imekabidhi mahitaji mbalimbali kwa ajili ya watoto hao, yakiwemo mchele, maharage, sabuni, juisi, mafuta ya kupikia, vitunguu, na mbuzi kwa ajili ya lishe na mahitaji ya kila siku.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Itunda, aliipongeza TPSC kwa maadhimisho yenye dhamira ya kugusa maisha ya watu. Alisema hatua hiyo inaonyesha utu na maadili ya utumishi wa umma yanayojengwa na chuo hicho.

"Chuo hiki kimeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa taifa letu kwa kutoa watumishi bora. Kila kinachofanywa hapa kinaonyesha dhamira ya kweli ya kuwahudumia wananchi na kujenga jamii yenye mshikamano," alisema Mhe. Itanda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampasi ya Mbeya, Ndugu Saidy Nzagamba, alisema chuo hicho kimeamua kushiriki na kusaidia watoto yatima kama sehemu ya kuwajengea faraja na kuwahakikishia kuwa jamii inawajali.

"Tunatambua changamoto wanazokabiliana nazo watoto hawa, ndiyo maana tumeamua kuwa jirani nao na kuwagusa kwa upendo. Huu ni mwanzo wa dhamira yetu kuendelea kushiriki shughuli za kijamii katika siku zijazo," alisema Nzagamba.

Viongozi wa vituo vya Iwambi na Bi Aisha Foundation waliushukuru uongozi wa TPSC Kampasi ya Mbeya kwa upendo na michango iliyotolewa, wakisema misaada hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika malezi na ustawi wa watoto.





















Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...