-Asema Serikali haitavumilia uzembe katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa kina kuhusu makadirio na matumizi ya fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa.

Ametoa agizo hilo leo Jumanne (Machi 10, 2026) wakati akizungumza na wananchi wa Kasanga, Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo, ambapo baadhi ya majengo bado hayajakamilika licha ya fedha kutolewa na Serikali.

Serikali ilitoa zaidi ya Sh. bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kalambo ambapo katika awamu ya kwanza majengo saba ya huduma za afya yalijengwa, ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la mama na mtoto, maabara, duka la dawa pamoja na miundombinu mingine ya huduma za hospitali. Hata hivyo, licha ya fedha hizo kutolewa na baadhi ya majengo kukamilika, majengo mawili muhimu ambayo ni jengo la theatre (chumba cha upasuaji) na wodi ya wanaume hayajakamilika.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu ameonesha kutoridhishwa na taarifa ya kuchelewa kukamilika kwa baadhi ya majengo ya hospitali hiyo.

“Ninyi mmeomba fedha, hamjapunguziwa hata senti moja ya fedha mlizoomba, mmepewa. Halafu mnapofika kwenye utekelezaji mnasema fedha haitoshi. Hii si sawa,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, Dkt. Mwigulu amemtaka Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Rukwa Bw. Mzalendo Widege kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama kulikuwa na uzembe au udanganyifu katika makadirio na matumizi ya fedha za ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo.

“Kamanda wa TAKUKURU nenda kachunguze, angalia kama kweli makadirio yalikuwa sahihi au kuna jambo lingine limejificha. Nipate taarifa ili tuweze kuchukua hatua stahiki,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali haitavumilia uzembe, ubadhirifu au ukiukwaji wa maadili katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuwa fedha zinazotolewa ni mali ya umma na zinapaswa kutumika kwa manufaa ya wananchi.

Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya ili kuboresha huduma za matibabu nchini.

Amesema katika kipindi cha takribani miaka minne, Serikali imejenga vituo vya afya zaidi ya 649 na zahanati zaidi ya 2,800 ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Pia Serikali imenunua vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa ikiwemo mashine za MRI katika hospitali za rufaa na CT Scan katika hospitali za mikoa.


Aidha, wataalamu zaidi ya 5,000 wa sekta ya afya wameajiriwa ndani ya siku 100 kama alivyoahidi Rais wakati wa kampeni za uchaguzi.






 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...