Ecobank Group imetangaza ukuaji mkubwa wa mikopo, likilenga kuimarisha ujasiriamali wa wanawake barani Afrika. Ecobank imerekodi ongezeko kubwa la asilimia 194 katika utoaji wa mikopo kwa biashara zinazoongozwa na wanawake, likifikia dola za Marekani milioni 780 mwaka 2025 kutoka dola milioni 265 mwaka 2024. Hatua hii inaashiria mafanikio ya juhudi za benki hiyo katika kukuza usawa wa kijinsia na kuimarisha uchumi wa ndani barani Afrika.

Taarifa hiyo ilitolewa wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Programu ya Jinsia ya Ecobank, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya International Women’s Day 2026.

Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa wanawake wajasiriamali wana mchango mkubwa katika kukuza ajira, kusaidia familia na kuimarisha minyororo ya thamani ya ndani. Hata hivyo, biashara nyingi zinazoongozwa na wanawake bado zinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mitaji, huku pengo la ufadhili likikadiriwa kufikia dola bilioni 42 barani Afrika.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Ecobank imeendelea kuwekeza katika mipango maalum inayolenga wanawake kwa kutoa mikopo rafiki, mafunzo ya biashara, ushauri na fursa za kuunganishwa na masoko ya kikanda. Lengo ni kuwasaidia wanawake kukuza biashara endelevu na zenye ushindani.

Moja ya mipango hiyo ni programu ya Ellevate, iliyoanzishwa mwaka 2020 kusaidia biashara za wanawake zilizoathiriwa na janga la COVID-19. Programu hiyo sasa imekua na kuwa moja ya miradi mikubwa zaidi barani Afrika, ikihudumia zaidi ya wanawake wajasiriamali 103,000 katika nchi 26. Zaidi ya wanawake 21,000 wamejiunga na mpango huo mwaka 2025 pekee, huku zaidi ya 24,000 wakinufaika na mafunzo na ushauri wa kibiashara.

Aidha, Ecobank imezindua programu ya MAMA inayolenga kuwasaidia wanawake wanaofanya biashara katika sekta isiyo rasmi, kwa kuwapatia mikopo nafuu na kuwasaidia kuingia katika mfumo rasmi wa kifedha. Mpango huo tayari umewafikia zaidi ya wanawake 10,000, huku zaidi ya 2,000 wakipata mikopo yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 1.8.

Katika juhudi za kuongeza upatikanaji wa mtaji, Ecobank pia ilizindua hati fungani maalum ya jinsia nchini Côte d’Ivoire mwaka 2025, iliyokusanya zaidi ya faranga za CFA bilioni 11 ndani ya saa 48. Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia kutoa mikopo kwa zaidi ya biashara 1,200 ndogo na za kati zinazomilikiwa na wanawake.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kundi la Ecobank, Jeremy Awori alisema wanawake wajasiriamali ni mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi wa Afrika, lakini bado wanakumbana na changamoto za upatikanaji wa fedha.

“Ecobank inaendelea kushughulikia changamoto hiyo kwa kuunganisha mitaji, ujuzi na fursa za masoko kupitia mtandao wake wa bara zima. Ongezeko hili linaonyesha wazi mahitaji makubwa ya huduma hizi na mafanikio ya programu zetu,” alisema.

Kwa siku zijazo, Ecobank inapanga kupanua zaidi programu ya Ellevate katika masoko yote inayofanya kazi, kuimarisha huduma zisizo za kifedha kama zana za kidijitali, pamoja na kuanzisha bidhaa mpya zitakazolenga wanawake ili kuongeza ushiriki wao katika uchumi wa Afrika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...