RAIS  Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekabidhi Tuzo za Viongozi Bora barani Afrika kwa Mwaka 2026 katika Hafla iliyofanyika Accra, Ghana tarehe 28 Februari 2026.

Tuzo hizo zinatolewa na Jarida la Africa Leadership Magazine linaloandaliwa na Taasisi ya Uongozi Afrika (Africa Leadership Organisation) ambayo Rais Mstaafu Dkt. Kikwete ni Mwenyekiti wa Bodi yake ya Ushauri.

Mshindi wa Jumla wa Tuzo hizo ni Rais John Dramani Mahama wa Ghana, ambaye ametunukiwa Tuzo ya Mwafrika wa Mwaka kwa Mwaka 2026 kwa kutambua mchango wake katika kukuza demokrasia na uchumi nchini Ghana pamoja na kuwa kinara katika kuimarisha utengamano wa kikanda kupitia Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA).

Akihutubia kabla ya kukabidhi Tuzo hiyo ya mshindi wa jumla, Rais Mstaafu Dkt. Kikwete ameeleza kuwa "kila kizazi za uongozi hukutana na changamoto za kipekee za wakati wake na hivyo hulazimika kubuni njia za kipekee za kuzitatua". Akaongeza kuwa "kipimo mojawapo cha mafanikio katika uongozi ni kuweza kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuboresha hali ya jumla ya kimaisha kwa watu unaowaongoza kutoka hali ya chini kwenda hali ya juu zaidi".

Mbali na Rais Mahama, miongoni mwa watu mashuhuri waliiopata Tuzo hizo ni pamoja na Waziri Mkuu wa Ufalme wa Lesotho, Samuel Matekane aliyepata tuzo kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi nchini Lesotho pamoja na Mkuu wa Majeshi wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba aliyepata tuzo kwa kutambua mchango wake katika kuliimarisha jeshi la Uganda na kukuza diplomasia ya kijeshi katika ukanda wa maziwa makuu.

Rais wa Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah alipata Tuzo ya Kiongozi Bora wa Kisiasa Afrika huku Makamu wa Rais wa Angola Esperança da Costa, Makamu wa Rais wa Angola akioata Tuzo ya Kiongozi Bora Mwanamke barani Afrika.

Tuzo ya Rais Mahama ilipokelewa kwa niaba yake na Mwanasheria Mkuu wa Ghana, ambaye pia ni Waziri wa Sheria wa Ghana, Dominic Akuritinga Ayine wakati tuzo ya Jenerali Kainerugaba ilipokelewa na Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda, Kanali Chris Magezi.

Kila mwaka Jarida la Africa Leadership Magazine huratibu mchakato wa wazi unaojumuisha kupokea mapendekezo ya viongozi mbalimbali wenye sifa ambao hupigiwa kura kwa njia ya mtandao ili kupata washindi. Viongozi wa tasnia mbalimbali zikiwemo uongozi wa kisiasa, diplomasia, biashara na uwekezaji, ujasiriamali, habari, ulinzi na usalama, nk., wanaoshinda hupokea Tuzo hizo kwa kutambua mchango wao katika kusimamia vizuri tasnia zao pamoja na kulea na kuwaandaa vijana wanaowaongoza ili kuja kuwa viongozi bora wa baadaye.

Katika hafla hiyo, jumla ya Tuzo 36 zilitolewa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...