NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO 

Kampeni ya "Soma na Mkarafuu," inayotekelezwa na Serikali ya Mkoa wa Morogoro, inatoa fursa mpya ya kiuchumi kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza Baada ya kuwapatia miche kumi ya  mkarafuu. 

Kampeni hii, ambayo inalenga kukuza kilimo cha zao la mkarafuu, inawapa wanafunzi na familia zao njia ya kujitegemea kifedha baada ya miaka minne, wakati ambapo zao hilo linapozalisha.


KILIMO CHA MKARAFUU NA FAIDA ZAKE KIMATAIFA

Mkarafuu ni zao lenye soko kubwa duniani, na linapandwa katika maeneo mbalimbali duniani kwa faida yake kubwa kiuchumi, kwa mujibu wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Musa Ali Musa, kila mkarafuu unazaa kilo tano na kuendelea na kilo moja inauzwa kati ya shilingi 15,000 hadi 20,000. 

"Miche ya mkarafuu inakua kwa kasi na inaanza kutoa mazao wakati mwanafunzi anapomaliza mtihani wa kidato cha nne, hivyo atakuwa na uwezo wa kujimudu kifedha akiwa katika kidato cha tano au anapojiunga na mafunzo ya ufundi," alisema Musa.

Kampeni hii ni muhimu si tu kwa kuongeza kipato kwa wanafunzi na familia zao, bali pia inahamasisha wanafunzi kufanya bidii katika masomo yao kwa kuwa wanajua kuwa wataweza kujimudu kifedha kupitia kilimo cha mkarafuu baada ya kumaliza masomo.

 Wanafunzi watakuwa na uhuru wa kuchagua ni njia gani ya maisha wanayotaka, bila kuathiriwa na changamoto za kifedha.


KUPUNGUZA NDOA ZA MAPEMA NA UTORO KWA WATOTO WA KIKE

Kampeni hii pia ina mchango mkubwa katika kupunguza utoro na ndoa za mapema, hasa kwa watoto wa kike. Kwa kuwa watoto wa kike sasa watakuwa na fursa ya kujitegemea kifedha, watakuwa na uwezo wa kugharamia masomo yao na kujiendeleza kimasomo, jambo ambalo linawapa uhuru zaidi wa kuchagua mustakabali wao. 

"Watoto wa kike, ambao mara nyingi walikosa fursa ya kujitegemea kutokana na ukosefu wa fedha, sasa watakuwa na njia ya kujimudu," aliongeza Katibu Tawala.

Fatuma Amri, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Tawa, ameeleza furaha yake kuhusu mpango huu wa kipekee, akisema, "Hii itatufanya tusome kwa bidii na kuwa na uhakika wa kuendelea na masomo yetu baada ya kidato cha nne. Hatuwezi tena kuwa na wasiwasi kuhusu ada na gharama za shule."

MAFAKIO YA KAMPENI NA MATUMAINI YA BAADAYE

Kampeni ya "Soma na Mkarafuu" inaonyesha mafanikio ya awali, na kwa mwaka 2026, jumla ya miche 2,650 ya kokoa iligawiwa kwa wanafunzi wa Halmashauri ya Mlimba, na miche 9,680 imetolewa kwa wanafunzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

 Miche hii ya kilimo itasaidia wanafunzi kujiendeleza kimasomo na kiuchumi baada ya kumaliza kidato cha nne.

Dkt. Rozalia Rwegasira, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali, anasema kuwa kampeni hii itasaidia kuinua uchumi wa familia na pia itawawezesha wanafunzi kuanzisha miradi ya kilimo itakayowaingizia kipato.

 "Miche ya mkarafuu itachangia katika kukuza uchumi wa wanafunzi na familia zao, na itakuwa na manufaa makubwa kwa mkoa na taifa kwa ujumla," alisema Dkt. Rwegasira.

MOTISHA KWA WANAJUMUIYA BORA

Serikali ya Mkoa wa Morogoro pia imeandaa motisha kwa wanafunzi watakaofanya vizuri katika utunzaji wa miche ya mkarafuu. Wanafunzi watakaofanya vizuri watajipatia zawadi za sare za shule, madaftari, na zawadi kubwa ya safari ya kwenda Zanzibar kwa mwanafunzi atakayefanya vizuri zaidi.








Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...