Na Mwandishi wetu -  Dodoma

Jeshi la Magereza Tanzania limehimiza matumizi sahihi ya takwimu za wafungwa na mahabusu kama nyenzo muhimu ya kupanga na kuboresha huduma za urekebishaji.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, CP Nicodemus Tenga, amesema takwimu hizo si tu ni hitaji la kitaifa bali pia zinazingatia viwango vya kimataifa vinavyolenga kuongeza uwazi na ufanisi katika taasisi za magereza.

Ameeleza kuwa uwepo wa takwimu sahihi husaidia kupanga mikakati madhubuti ya kuwahudumia wafungwa na mahabusu, ikiwemo masuala ya afya, makazi, lishe na programu za urekebishaji. Pia hutoa mwanga kwa watunga sera kutambua changamoto na kuzitatua kwa wakati.

CP Tenga amesisitiza wataalamu wa takwimu kuhakikisha taarifa wanazokusanya zinatumika kwa vitendo, akibainisha kuwa takwimu zisipotumika hupoteza maana na thamani yake kwa taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Tafiti na Takwimu wa Jeshi la Magereza, DCP Justine Kaziulaya, amesema mwaka 2025 jumla ya wafungwa na mahabusu walifikia 23,940, ambapo wafungwa walikuwa 19,646 na mahabusu 4,294.

Aidha, amebainisha mikakati mbalimbali ya kupunguza uhalifu ikiwemo utoaji wa mafunzo ya ufundi, programu za kisaikolojia, tiba ya uraibu pamoja na kuimarisha ushirikiano na jamii na matumizi ya teknolojia za kisasa.

Naye Meneja wa Tafiti na Ubunifu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Bi. Mariam Kitembe, amesema serikali inaendelea kuimarisha sekta ya takwimu kupitia mpango wa TSMP II, ambao unalenga kuongeza ubora na matumizi ya takwimu katika taasisi mbalimbali zikiwemo magereza.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...