Mastercard leo imefanya ziara yake maalumu katika makao makuu ya Benki ya Exim Tanzania jijini Dar es Salaam, kuimarisha zaidi ushirikiano wa kimkakati kati ya taasisi hizo na kukabidhi tuzo mbili muhimu kutokana na mafanikio ya Benki hiyo kwa mwaka 2025.
Katika ziara hiyo, Benki ya Exim ilitunukiwa tuzo ya “Best Elite Banking Proposition - 2025” pamoja na tuzo ya “Highest Spend Per Card in Tanzania - 2025”, zikionesha mafanikio yake katika kubuni na kuendesha huduma za kibenki za hadhi ya juu pamoja na kuongoza kwa matumizi ya kadi nchini Tanzania.
Tuzo hizi zinatokana na mafanikio yaliyopatikana kufuatia uzinduzi wa huduma ya Elite Banking mnamo Julai 2025, huduma iliyolenga kuwahudumia wateja wa hadhi ya juu (High-Net-Worth Individuals) kwa suluhisho za kifedha zilizobuniwa mahsusi kulingana na mahitaji yao kulingana na mfumo wao wa maisha. Kupitia huduma hii, wateja wanapatiwa Meneja Mahusiano binafsi, anayetoa suluhisho za uwekezaji na mikopo kwa ajili ya mtu binafsi, pamoja na kufaidika na ofa ya kimataifa ikiwemo upatikanaji wa lounge za viwanja vya ndege kupitia Mastercard DragonPass.
Aidha, tuzo ya “Highest Spend Per Card” inaonesha mafanikio ya Benki katika kuhamasisha matumizi ya kadi kwa wateja wake, hatua iliyochangiwa na kampeni mbalimbali za kimkakati ikiwemo UEFA Priceless Campaign, ambayo ilihamasisha malipo kwa kutumia kadi huku ikitoa fursa za kipekee za kufurahia ofa za kimataifa kwa washindi wake.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo hizo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya Exim Tanzania, Andrew Lyimo, alisema:
“Tuzo hizi kutoka Mastercard ni uthibitisho wa mkakati wetu wa kubadilisha na kuinua viwango vya huduma za kibenki za hadhi ya juu nchini Tanzania. Uzinduzi wa Elite Banking mwaka 2025 ulikuwa hatua muhimu katika safari yetu ya kuwahudumia wateja wetu kwa ubora wa hali ya juu, kwa kuunganisha suluhisho za kifedha zilizo bora na ofa za kipekee kulingana na mfumo wa maisha ya wateja wetu. Mafanikio haya yanatokana na imani ya wateja wetu pamoja na uwekezaji wetu endelevu katika ubunifu na teknolojia.”
Kwa upande wake, Makamu Raisi na Meneja wa akaunti wa Master Card, Elsie Kaguru alisema:
“Benki ya Exim imeonesha uongozi wa kipekee katika kukuza huduma za “premium Banking” na kuimarisha matumizi ya kadi nchini Tanzania. Ukuaji wa haraka wa huduma ya “Elite Banking” pamoja na kiwango cha juu cha matumizi kwa kila kadi vinaakisi uelewa sahihi wa mahitaji ya wateja wa kisasa. Tunajivunia ushirikiano wetu na Benki ya Exim na tuna matarajio makubwa ya kuendeleza mafanikio haya kwa pamoja.”
Ushirikiano kati ya Exim Bank na Mastercard umejikita katika kuimarisha mifumo salama ya malipo ya kidijitali, kuboresha huduma za kadi za hadhi ya juu, na kupanua upatikanaji wa manufaa ya kimataifa kwa wateja wa Tanzania. Ushirikiano huu umeleta matokeo yanayoonekana katika utofautishaji wa bidhaa pamoja na ongezeko la utendaji wa miamala.
Ziara hiyo imeendelea kuonesha dhamira yao ya pamoja ya taasisi hizi mbili katika kukuza malipo ya kidijitali, kuimarisha huduma za kibenki za hadhi ya juu, na kuchochea ukuaji endelevu wa sekta ya fedha nchini Tanzania.
Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Shani Kinswaga, akipokea moja ya tuzo mbili kutoka kwa Makamu wa Rais Mwandamizi – Meneja wa Nchi, Afrika Mashariki na Visiwa vya Bahari ya Hindi wa Mastercard, Shehryar Ali (wa pili kushoto), wakati wa ziara ya Mastercard katika ofisi za Benki hiyo jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii. Benki ya Exim ilitunukiwa tuzo ya “Best Elite Banking Proposition - 2025” pamoja na tuzo ya “Highest Spend Per Card in Tanzania - 2025”. Tukio hilo lilishuhudiwa na Makamu wa Rais na Meneja wa Akaunti wa Mastercard, Elsie Kaguru (kushoto), Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na wa Kati wa Benki ya Exim Tanzania, Andrew Lyimo (wa pili kulia), pamoja na Mkuu wa Uendeshaji na Utoaji wa Huduma wa Exim Benki, Tumaini Mwakafwa…




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...