Na Mwandishi Wetu, Lindi
Serikali imezindua rasmi Jukwaa la Majadiliano ya Biashara kwa Biashara (B2B) likiwa na lengo la kuchochea uwekezaji, kuongeza thamani ya rasilimali za misitu na kuimarisha uhifadhi nchini, huku ikisisitiza kuwa misitu ni msingi wa maisha na uchumi endelevu.
Uzinduzi huo umefanyika leo Machi 18, 2026 katika Uwanja wa Ilulu, Manispaa ya Lindi, ukiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na kampeni ya kitaifa ya upandaji miti inayotarajiwa kufikia kilele Machi 21, 2026.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, amesema uhifadhi wa misitu si chaguo bali ni hitaji la msingi kwa ustawi wa binadamu na uchumi wa taifa.
“Bila kuhifadhi hatuna maji, bila kuhifadhi hatuna maisha. Tunapozungumzia uhifadhi, tunazungumzia uhai wa binadamu na mustakabali wa vizazi vijavyo,” amesema Mhe. Telack.
Amesema jukwaa hilo ni fursa muhimu ya kuwakutanisha wadau wa sekta ya misitu, wafanyabiashara na serikali ili kujadili namna bora ya kutumia rasilimali hizo kwa tija bila kuathiri mazingira.
Katika hatua nyingine, Mhe Telack amesisitiza umuhimu wa Mkoa wa Lindi katika sekta ya misitu, akibainisha kuwa mkoa huo una mchango mkubwa katika uzalishaji wa mazao ya misitu, ikiwemo mbao ngumu na mikorosho.
“Mkorosho ni msitu. Tukikata mikorosho na kuona maghorofa pekee, ujue tumefilisika,” ameonya.
Aidha, amepongeza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na upandaji miti nchini, akimtaja kuwa kinara wa ajenda hiyo.
Kwa upande wake, msimamizi wa mjadala huo, Dkt. Siima Salome Bakengesa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, amesema jukwaa hilo linalenga kuunganisha fursa za biashara kupitia mifumo ya B2B na B2G ili kuongeza mchango wa sekta ya misitu katika uchumi.
“Hapa tunalenga kuweka mazingira wezeshi ili sekta ya misitu na nyuki iweze kutoa thamani kubwa zaidi kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” amesema.
Ameongeza kuwa mada nane zimeandaliwa kujadili masuala muhimu ikiwemo biashara ya kaboni, matumizi ya teknolojia, sera na kanuni pamoja na namna ya kuongeza thamani ya mazao ya misitu.
Uzinduzi huo unatangulia tukio kubwa la kitaifa la ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Kampeni ya Upandaji Miti Kitaifa, unaotarajiwa kufanyika kesho Machi 19, 2026 katika Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Emmanuel Nchimbi, atakayeongoza uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya upandaji miti.
Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kaulimbiu “Misitu ni Uchumi Endelevu, Tuihifadhi kwa Maendeleo ya Taifa,” yakilenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi na wadau katika uhifadhi wa misitu na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kampeni ya upandaji miti kama nyenzo ya kurejesha uoto wa asili, kulinda vyanzo vya maji na kuimarisha uchumi wa kijani, huku Lindi ikitajwa kuwa moja ya mikoa yenye mchango mkubwa katika rasilimali za misitu nchini.















Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...