Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameielekeza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuendelea kusimamia ubora wa elimu inayotolewa na kuzuia madhara yanayohatarisha usalama wa watu na uchumi wa nchi.

Akizindua bodi mpya ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), leo Machi 6,2026, Dar es Salaam, Profesa Mkenda amesema katika kusimamia taasisi za utoaji elimu ya vyuo vya juu, tume inapaswa ifanye kazi ya kuwezesha na kusaidia wawekezaji wanaotaka kuanzisha vyuo Vikuu Tanzania kufikia ubora na viwango viwango vinavyotakiwa.

Pia amewataka Makamishna kuimarisha ubora wa elimu ya chuo kikuu nchini.

Usinduzi wa Bodi hiyo unaashiria mwanzo wa muhula mpya wa uongozi wa Bodi hiyo ambayo Mwenyekiti ni Prof. Makenya Maboko.

Akizungumza katika uzinduzi huo Profesa Mkenda amesema kuna wakati wanalaumiwa kwa kusimamia ubora, lakini wasiposimamia madhara yake ni makubwa kwa mfano vyuo vya madaktari kuna utaratibu wanapotoa shahada za udaktari, wanahitaji wanafunzi wangapi, maabara ngapi, walimu na madaktari wa aina gani.

"Tume imebeba jukumu kubwa la kulinda ubora wa elimu ya juu pamoja na imani ya umma katika vyuo vikuu, vyetu” amesema Prof. Mkenda.

Ameeleza kazi hizo hazifanywi na tume pekee bali hushirikisha na mabaraza ya madaktari na vigezo vingine vya Afrika Mashariki.

Ameongeza iwapo mwekezaji akitaka kukiuka ili kupata faida, matokeo yake ni kupata wahitimu ambao wataumiza watu katika kutibu.

Amesisitiza vigezo vya utoaji tiba nchini ni rahisi kuliko vilivyowekwa na Afrika Mashariki na kwamba hawapaswi kuvilegeza zaidi na badala yake kufikia vigenzo vya jumuiya hiyo.

"Tume hii ihakikishe inaufanisi wa kujibu malalamiko na kuwatembelea wadau wao ili kuzuia madhara yatokanayo na kutozingatia vigezo vya ubora ikiwemo uchumi wa nchi, usalama wa watu," amesisitiza.

Halikadhalika, Waziri Mkenda amesema kuwa vyuo vikuu vinapaswa kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia mifumo ya utawala bora sambamba na taratibu za uthibiti wa ubora wa elimu ili kupata wahitimu wenye elimu, maarifa, ujuzi na uwezo wa kustahimili ushindani kitaifa, kikanda na kimataifa.

Pia ameitaka tume hiyo kuongeza ufanisi katika mawasiliano, kuhimizana kutembelea maeneo ambayo wawekezaji wanataka kuanzisha vyuo vikuu na wawape ushauri

Akizungumza kwa niaba ya Tume, Prof. Maboko ameishukuru Serikali kwa imani iliyoiweka kwa Tume hiyo. Amesema kuwa Bodi itashirikiana kwa karibu na Sekretarieti ya Tume katika kuimarisha mifumo ya ndani ya uthibiti wa ubora wa elimu ya chuo kikuu pamoja na uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa vyuo vikuu ili kuimarisha ukuaji na maendeleo endelevu ya elimu ya chuo kikuu nchini.

“Jukumu letu si la kiutawala pekee,” amebainisha Prof. Maboko. “Ni wajibu wa kimkakati kuhakikisha elimu ya chuo kikuu nchini inabaki kuwa yenye kuaminika, yenye ushindani na inayokidhi mahitaji ya soko la kitaifa, kikanda na kimataifa.”

Hafla ya uzinduzi huo, ilitanguliwa na warsha ya Makamishna wa TCU iliyofanyika tarehe 5 hadi 6 Machi 2026. Warsha hiyo ya kimkakati ilijikita katika kutathmini hali ya elimu ya chuo kikuu nchini kwa kulinganisha mfumo wa elimu ya juu wa Tanzania na mifumo ya elimu ya juu katika nchi za Afrika ikiwemo Mauritius, Afrika Kusini na Kenya.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...