Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa meli nne kubwa za mizigo katika Bandari ya Karema kunatarajiwa kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma, pamoja na kuimarisha biashara katika ukanda wa Ziwa Tanganyika na nchi jirani.

Hadi sasa utekelezaji wake umefikia zaidi ya asilimia 95, huku meli zote zikiwa tayari zimeingizwa majini na zipo katika hatua za mwisho za uhakiki kabla ya kuanza kutoa huduma rasmi za usafirishaji wa mizigo.

Akizungumza wakati wa tukio la kuingizwa majini kwa mara ya kwanza meli ya nne, Msimamizi Msaidizi wa Bandari ya Karema, Anthony Poyo, amesema kukamilika kwa meli hizo kutaimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Zambia.

Poyo amesema meli hizo pia zinatarajiwa kuwa kichocheo muhimu katika usafirishaji wa madini mbalimbali kama lithium, shaba na dhahabu yanayochimbwa katika eneo la Manono nchini DRC. Madini hayo yatasafirishwa kupitia Manono hadi Bandari ya Kalemie, kisha Bandari ya Kigoma kabla ya kuendelea hadi Bandari za Dar es Salaam na Tanga kwa ajili ya kusafirishwa kwenda masoko ya kimataifa.

Ameongeza kuwa uwepo wa meli hizo utasaidia pia sekta ya kilimo kwa kuwa wakulima watapata urahisi wa kusafirisha mazao yao kwenda katika masoko ya ndani na ya kikanda, hatua itakayosaidia kuongeza thamani ya mazao na kipato cha wananchi.

Kwa mujibu wa Poyo, mradi huo pia utachochea ajira kwa Watanzania, hususan katika sekta ya ubaharia, ambapo kila meli inahitaji angalau mabaharia 15.

Aidha, shughuli nyingine za kiuchumi kama upakiaji na upakuaji wa mizigo, huduma bandarini pamoja na biashara ndogondogo zinazozunguka bandari zinatarajiwa kuongezeka.

“Ujenzi wa meli hizi umetokana na juhudi za Serikali kufungua fursa za uwekezaji.

Mradi huu umefungua milango mipya ya kiuchumi kwa taifa na wananchi mmoja mmoja,” amesema Poyo.

Ameeleza pia kuwa uwepo wa miundombinu ya reli ya kisasa ya SGR pamoja na reli ya MGR utaongeza ufanisi katika usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Karema kwenda Bandari za Dar es Salaam na Tanga.

Kwa upande wake, Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Ankola Shipyard Co. Ltd, Mohammed Mohamed Chande, amesema mradi huo umefungua fursa nyingi za ajira kwa vijana tangu ulipoanza, huku wengi wao wakipata ujuzi na uzoefu katika sekta ya ujenzi wa meli.

Chande amesema licha ya changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi, waliweza kuzidhibiti na kufanikisha ujenzi huo kwa wakati uliopangwa.

Baadhi ya wananchi wa maeneo yanayozunguka Bandari ya Karema wameipongeza Serikali na wawekezaji kwa kukamilisha mradi huo wakieleza kuwa utasaidia kupanua masoko ya mazao ya kilimo, samaki na mifugo, pamoja na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazozunguka Ziwa Tanganyika.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...