Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Zege la Gagi linalojengwa Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga kupitia Mfuko wa Dharura (CERC) limeondoa adha ya usafiri iliyokuwa inawakabili kwa muda mrefu wananchi wa Kata hiyo na maeneo ya jirani. 

Daraja hilo lenye urefu wa mita 11.2 na upana mita 8.2 linajengwa kwenye barabara ya Gagi ambalo linaunganisha Kata za Ndembezi na Ngokolo  katika Manispaa hiyo.

Akizungumza kwenye mahojiano maalum katika ziara ya kutembelea mradi huo, Diwani wa Kata ya Ndembezi na Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Upendo John Sawa amesema kukosekana kwa daraja hilo ni kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa Kata hiyo kutokana na ugumu wa kupita katika eneo hilo hasa kipindi cha masika kutokana na kivuko cha awali kusombwa na maji.

"kipindi cha masika akina mama walikuwa wanajifungulia hapa, wanafunzi kwenda shule mpaka wapatikane watu wa kuwavusha, wengine wanavushwa kwa pesa, Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa na wajumbe wake walikuwa wanakaa hapa kusubiri kuwavusha watoto ilikuwa ni adha kubwa sana" .

Amesema kwa hatua iliyofikia ya ujenzi wa daraja hilo ni furaha kubwa sana kwao na kwamba kilio cha wakazi wa Butengwa kimeisha na kuongeza kuwa daraja hilo limeleta tabasamu kwa wakazi wa mtaa wa Botengwa na Kata ya Ndembezi kwa ujumla.

Naye Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Samson Pamphili amesema kuwa wakati wa masika eneo hilo lilikuwa halipitiki kutokana na mafuriko makubwa ambayo yalisababishwa na mvua hivyo walilipa kipaumbele kwenye mipango yao kwa kujenga daraja kupitia chanzo chochote cha pesa.

Amesema wamebahatika kupata fedha za kutekeleza kazi hiyo kiasi cha shilingi 105,477,950 kupitia Mfuko wa Dharura (CERC) ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia na unalenga kuboresha miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mafuriko.  

Ameongeza kuwa muda wa ujenzi wa daraja hilo ni miezi sita na kwamba ujenzi ulianza Desemba 29, 2025 na unatarajia kukamilika Juni 28, 2026 lakini kwa mujibu wa Mhandisi Pamphili ujenzi wa daraja hilo umefanyika kwa haraka na mpaka sasa umefikia asilimia 93 na ifikapo Machi 28, 2026 daraja hilo litaanza kutumika.

Kwa upande wake Emmanuel Exavery Hanya Mkazi wa mtaa wa Botengwa amesema eneo hilo lilikuwa ni tishio  kabla ya ujenzi wa daraja hilo na kuongeza kuwa walikuwa wakipata shida kuvuka eneo hilo kipindi cha masika hasa wanafunzi kwenda shuleni, akina mama wajawazito na waliokuwa wakienda kwenye shughuli zao za kiuchumi. 

"Tunaishukuru serikali kwa usikivu wao kwa kuja kutatua changamoto iliyokuwepo kwenye eneo hili na kufikia hatua hii, hivyo changamoto kwenye eneo hili zimeisha na wananchi tunaweza kuvuka bila shida yeyote".







Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...