Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa hiari kwa taasisi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi nchini, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imetoa onyo kwa watakaoshindwa kutimiza takwa hilo kwa wakati.

Kupitia mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Machi 26, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Dkt. Emmanuel Lameck Mkilia, alisisitiza kuwa mwisho wa usajili wa hiari ni tarehe 8 Aprili, 2026, huku hatua za kisheria zikianza rasmi siku inayofuata, Aprili 9.

Dkt. Mkilia alieleza kuwa serikali imetoa muda wa kutosha kwa taasisi kujiandaa tangu mwaka 2024, ambapo mchakato huo ulianza rasmi kufuatia uzinduzi wa Tume hiyo. Aliongeza kuwa muda huo uliwahi kuongezwa mara mbili ili kutoa nafasi zaidi kwa wadau kutekeleza matakwa ya sheria.

“Hatua zinazofuata ni utekelezaji kamili wa sheria. Taasisi yoyote itakayobainika kutokujisajili itachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, mtu binafsi anayekiuka masharti anaweza kutozwa faini kuanzia shilingi laki moja hadi milioni 20 au kifungo kisichozidi miaka 10 jela. Kwa upande wa taasisi na makampuni, adhabu inaweza kufikia faini ya hadi shilingi bilioni tano, kulingana na uzito wa kosa.

Sheria hiyo inahusu sekta mbalimbali muhimu, zikiwemo taasisi za serikali, benki, kampuni za bima, hospitali, taasisi za elimu, kampuni za mawasiliano, viwanda, pamoja na sekta za utalii, usafirishaji na nyinginezo.

PDPC imewataka wadau wote ambao bado hawajakamilisha usajili kufanya hivyo haraka kabla ya muda uliowekwa kuisha, ili kuepuka madhara ya kisheria yatakayoanza kutekelezwa bila kusita.










 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...