Na: Dkt. Reubeni Lumbagala, Tanga

Watoto wana haki zao za msingi. Wanapaswa kupendwa, kulindwa, kusikiliza, kupewa malezi na matunzo. Pia, watoto wanapaswa kupewa mahitaji yote ya msingi yaani chakula, mavazi na malazi. Kimsingi, ni wajibu wa msingi kwa wazazi na walezi hukakikisha watoto wanapata haki na mahitaji yao muhimu ili waweze kufurahia maisha kwa kuzingatia kuwa watoto ni kiungo muhimu katika familia na maendeleo ya Taifa.

Serikali kama mdau muhimu wa ustawi na maendeleo ya watoto, inawajibika kuweka mazingira mazuri ya ustawi wa watoto. Aidha, serikali inawajibika kutunga sheria zitakazowalinda watoto ili kesho zao ziweze kutimia na Taifa linufaike kupitia uwepo wao. Ipo changamoto katika jamii zetu kwa baadhi ya wanawake kutupa watoto pindi wanapojifungua watoto hao. 

Wengine huwatupa katika mazingira ambayo ni rahisi kuokotwa na wapita njia lakini baadhi yao huwatupa katika mazingira mabaya mathalani jalalani ambapo kwa bahati mbaya wengine huokotwa wakiwa tayari wameshapoteza maisha. Mbaya sana.

Kwa sababu yeyote ile, suala la kutupa mtoto si suala zuri hasa mtoto anapotupwa katika mazingira mabaya ambayo yanazalisha matatizo mengine mathalani magonjwa kutokana na kupigwa baridi kali na wengine kupoteza maisha kabisa.

 Zipo sababu kadhaa zikiwemo suala la hali ngumu za maisha au baba mzazi wa mtoto kukataa mimba au kumlea mtoto, na hivyo mwanamke kuamua kumtupa mtoto wake aliyehangaika nae kwa miezi tisa tumboni na uchungu wa kumzaa hospitalini.

Januari 17, 2026, karibu na nyumba ya wageni (Guest House) ijulikanayo kwa jina la Kasulu, Nzega Mjini mkoani Tabora, alitelekezwa mtoto ambapo Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Nzega chini ya uongozi wa Mkuu wa wilaya hiyo, Naitapwaki Tukai pamoja na Jeshi la Polisi wilaya ya Nzega waliamua kumchukua mtoto huyo na kumpeleka hospitali kwa uchunguzi na uangalizi huku jitihada za kumpata mama mzazi wa mtoto huyo zikiendelea.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa upendo mkubwa alionao kwa watoto na jamii, ameamua kumchukua mtoto huyo ambaye amepewa jina la Grace Samia Suluhu Hassan. Tukio hilo la upendo limefanyika Machi 11, 2026, katika makazi yake ya Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma. Kipekee kabisa, nimpongeze Rais Dk. Samia kwa moyo wake wa upendo kwa mtoto huyo kwa kuamua kuchukua jukumu la kumuasili awe ni sehemu ya watoto na familia yake kimalezi na kimatunzo.

Rais Dk. Samia anatoa matumaini mapya juu ya hatma ya mtoto huyo kuwa yupo kwenye mikono salama na Mwenyezi Mungu amjalie mtoto huyo afya njema ili akue vizuri. "Wanaotupa watoto hawajui wanalolifanya. Kuliko kumtupa mtoto ni afadhali ukamkabidhi katika mamlaka za kisheria au kituo cha kulelea watoto. Kila mtoto aliyezaliwa ni hazina na hatujui kesho yake," amesisitiza Rais Dk . Samia.

Pengine ni muda muafaka kwa wanaume kutimiza majukumu ya kimalezi badala ya kutelekeza familia, na hivyo kuwaachia wanawake njia panda, hali inayosababisha baadhi ya wanawake kufikia hatua ya kuwatupa watoto. 

Lakini jambo la muhimu ambalo Rais Dk. Samia amelisisitiza ni kutumia vituo vya watoto kuomba msaada ya kulelewa mtoto badala ya kumtupa mtoto, jambo ambalo si zuri hata mbele za Mungu na hata katika maadili yetu ya Kitanzania. Kwa hakika, Rais Dk. Samia ameonyesha upendo wa kipekee kwa jamii kwa kumuasili mtoto Grace Samia Suluhu Hassan. Tumuombee mtoto Grace Samia Suluhu Hassan awe na afya njema na siku moja aje kuwa nguzo muhimu kwa nchi yetu ya Tanzania.

Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu katika Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.

Maoni : 0620 800 462.







Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...