Na Khadija Kalili, Kibaha
MWENYEKITI wa Baraza la Wafanyakazi Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa huo, Pili Mnyema, amewataka wajumbe wa baraza hilo kujadili ajenda zenye tija kwa wananchi pamoja na kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Mnyema ameyasema hayo leo, Machi 3, 2026, wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi Mkoa wa Pwani kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kibaha.
Aidha, amesisitiza uwajibikaji, kufanya kazi kwa nidhamu na uadilifu, pamoja na kuhimiza ushirikiano ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Niwapongeze kwa mafanikio yaliyofikiwa, kwani Mkoa wa Pwani unaongoza katika mambo mengi yaliyoiwezesha kuwa kinara katika sekta mbalimbali. Hivyo, niwaombe tuendelee kushirikiana ili kuendeleza mafanikio hayo na kuufanya Mkoa wetu kuwa kinara katika kila sekta,” amesema Mnyema.
Katika hatua nyingine, amewataka wajumbe wa baraza hilo kuipa kipaumbele ajenda ya uwekezaji kwa kufanya kazi kwa ushirikiano, akieleza kuwa Mkoa wa Pwani ni mkoa wa kimkakati katika uwekezaji wa viwanda.
Aidha, kikao hicho kilipata fursa ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mpango wa bajeti wa mwaka 2025/2026, pamoja na kupokea na kupitisha rasimu yexa mpango wa bajeti ya mwaka 2026/2027. Vilevile, kilifanya uchaguzi wa Katibu na Katibu Msaidizi, ambapo Ramadhani Mwaiganju amechaguliwa kuwa Katibu, huku Mwajuma Mohamed amechaguliwa kuwa Katibu Msaidizi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...