Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rose Senyamule, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao wakati wa msimu wa mvua ili kuepuka ajali zinazoweza kusababisha vifo, kufuatia watoto wawili wadogo kufariki dunia baada ya kuzama kwenye madimbwi ya maji.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua maeneo yaliyoathiriwa na mvua Kata ya Nzuguni Halimashauri ya Jiji la Dodoma, leo Machi 13, 2026, amesema ni muhimu kwa wazazi kuhakikisha watoto hawachezi kwenye madimbwi au maeneo yenye maji mengi kipindi hiki cha mvua ili kuwalinda dhidi ya hatari zinazoweza kutokea.

Aidha, amewataka wananchi kutunza mazingira na kuepuka kuchafua mifereji ya maji kwa kutupa taka ovyo, akieleza kuwa hali hiyo huchangia kuziba mifereji na kusababisha maji kujaa katika makazi ya watu pamoja na barabarani.

Amesema pamoja na changamoto zinazosababishwa na mvua, bado wananchi wanapaswa kuona kuwa mvua ni neema kwa Jiji la Dodoma kwa kuwa inaongeza uzalishaji wa chakula na kuleta ukijani kwenye mazingira.

Katika hatua nyingine, amewataka baadhi ya wananchi waliovamia na kujenga kwenye njia za maji kuzingatia sheria za mipango miji ili kuepusha madhara yanayotokea wakati wa mvua, ikiwemo nyumba kujaa maji.

Ametoa pole kwa wananchi waliokumbwa na athari za mvua na kuwataka kuwa na uvumilivu wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kutatua changamoto hizo. Amesema suluhisho la kudumu litatekelezwa mara mvua zitakapopungua kunyesha ili kuruhusu utekelezaji wa maboresho ya miundombinu ya barabara na mifereji ya maji.

Akisoma taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Mtendaji wa Kata ya Nzuguni, Edgar Fungo, amesema kuanzia Januari 21, 2026 hadi Machi 13, 2026, jumla ya kaya 271 zimeathirika na maafa ya mvua katika kata hiyo. Kati ya hizo, nyumba 42 zimeezuliwa na upepo, nyumba 170 zimeingiliwa na maji na nyumba 59 zimebomoka.

Ameeleza kuwa mvua kubwa iliyonyesha Februari 9, 2026 iliathiri maeneo ya Mtaa wa Kitelela, Nzuguni C na Mahomanyika ambapo katika eneo la Kitelela barabara ziliharibika na kusababisha kushindwa kupitika, hali iliyosababisha wanafunzi kushindwa kwenda shule baada ya korongo kujaa maji pamoja na wananchi kukosa huduma za msingi.

Kwa upande wa Mahomanyika, daraja lilivunjika na kusababisha shughuli mbalimbali kusimama, huku katika eneo la Nzuguni C mfereji wa maji uliochimbwa kuzunguka ukuta wa Nane Nane ulijaa na kusababisha maji kusambaa hadi kwenye makazi ya wananchi.

Aidha, amesema Mbunge wa Jimbo la Mtumba, Anthony Mavunde, kwa kushirikiana na uongozi wa kata pamoja na diwani wa kata hiyo walitembelea maeneo yaliyoathirika na kutoa pole kwa wananchi pamoja na kusikiliza changamoto zao.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali, viongozi wa eneo pamoja na taasisi mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaopata madhara wanapatiwa msaada na hatua za kudumu zinachukuliwa ili kupunguza athari za mafuriko katika maeneo hayo siku zijazo.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...