Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Njombe

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umetoa rai kwa sekta binafsi nchini kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika miradi midogo ya kuzalisha umeme vijijini kwani wakala huo upo tayari kushirikiana nao kwa kila hatua.

Rai hiyo imetolewa leo Machi 11,2026 na Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yessaya mbele ya Wahariri wa vyombo vya habari ambao ni Wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF)walioko katika ziara ya kutembelea miradi inayosimamiwa au kufadhiliwa na wakala huo mkoani Njombe.

Wahariri hao wamepata nafasi ya kuona mradi wa kuzalisha umeme wa kilovati 317 uliopo kwenye Kijiji cha Boimanda katika kata ya Matola wilayani Njombe mkoani Njombe ambapo REA wametoa ruzuku ya Sh.bilioni 5.4 kujenga miundombinu ya mradi huo unaosimamiwa na Shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent

“Miradi ya uzalishaji umeme inayotekelezwa na sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini.Hivyo tunaendelea kutoa rai kwa sector binafsi kushiriki katika miradi ya aina hii hasa katika mikoa kama Iringa,Njombe na Ruvuma ambako kuna vyanzo vya maji vinavyoweza kutumika kuzalisha umeme.”

Kuhusu mradi huo wa umeme wa maji Mhandisi Yessaya amesema hadi sasa ujenzi wa miundombinu ya mradi huo umekamilika na kilichobaki ni kuwasha mtambo na kuunganisha umeme katika gridi ya taifa.

Amefafanua kuwa “Mradi huu ulianzishwa kuzalisha umeme kwa matumizi ya shirika ambalo linashughuli mbalimbali zinazohitaji umeme ikiwemo katika hospitali, shule, karakana na gereji.Baadae ulipanuliwa ili kunufaisha jamii kwa kuunganisha vijiji vitatu vya Matola, Boimanda na Kitulila.Hata hivyo REA tulishapeleka umeme katika Vijiji vyote vya Mkoa wa Njombe.”

Wakati huo huo Mratibu wa Mradi wa kuzalisha umeme wa Lupali, Sister Imaculatha Mlowe, amesema REA imechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha kukamilika kwa mradi huo kwani amekuwa Mdau muhimu tangu hatua za awali.

Pia amesema kwa hivi sasa zaidi ya wananchi 212 wa Kijiji cha Boimanda wanapata huduma ya umeme wa TANESCO wakati wananchi 366 wa Kijiji cha Matola wanapata umeme kupitia mradi wa zamani wa Lupali.

Aidha amesema mkataba wa kuuza umeme kati ya TANESCO na Shirika la St. Benedictine of Imiliwaha tayari umeshasainiwa na kazi ya kuanza uzalishaji zinatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ijayo.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...