Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha

SERIKALI imesema vikundi vya Malezi na Makuzi vinavyoendelea kuanzishwa nchini vimekuwa chachu ya kupunguza tatizo la ukatili wa watoto kwa kuongeza ulinzi na usalama dhidi yao.

Aidha jamii imetakiwa kuungana kwenye suala zima la malezi na makuzi ya mtoto na kwamba Baba anapaswa kuungana na mke wake kuhakikisha mtoto anapata malezi bora, salama na yenye upendo tangu mimba inapotungwa.

Akizungumza kwenye kongamano lililokutanisha makundi ya malezi na makuzi yaliyoko chini ya  taasisi ya malezi ya SOS Children's Village kutoka katika Halmashauri nne za Mkoa wa Arusha za Meru, Arusha DC, Karatu na Jiji, Machi 16 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Seleman Msumi, amesema kuwa malezi bora kwa watoto ni nguzo muhimu katika kuhakikisha jamii inapata maendeleo endelevu na yenye ustawi.

Amesema kuwa serikali inaendelea kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali ili kuhakikisha mwongozo wa malezi bora unatekelezwa kwa ufanisi katika jamii.

Msumi  amesema ushirikiano wa familia na jamii kwenye makuzi ya mtoto  utasaidia kupunguza vitendo vya ukatili vinavyotokea katika jamii, hasa kwa watoto, kwa kuwa jamii itakuwa na uelewa mpana kuhusu wajibu wa malezi na ulinzi wa mtoto.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee, wanawake na Makundi Maalum, Victor Rugarabamu, amesema uwepo wa makundi ya malezi ni mkakati wa Serikali wa kuwa na vikundi aki2 kote nchini ifikapo mwakani.

Amesema pamoja na mafanikio ya uanzishwaij wa makundi hayo, bado takwimu za uanzishwaji wake ni ndogo ambapo Hadi kufikia mwaka huu ni makundi 4060 pekee ambayo yameshaanzishwa nchini.

“ Mpaka Sasa takwimu zinaonyesha tuna vikundi vya Malezi na Makuzi 4060 pekee kote nchini wakati matarajio ni kuwa na vikundi laki2, kasi bado ni ndogo sana inapaswa kuongeza kasi zaidi Ili kufikia malengo,” amesema.

Aidha amelipongeza shirika la SOS Children’s Village kwa juhudi zake za kuanzisha vikundi vya malezi na Makuzi  katika mkoa wa Arusha na kutoa wito kwa taasisi na mashirika mengine kuungana na Serikali kuanzisha vikundi hivyo.

Amesema vikundi hivyo vina mchango mkubwa katika kuhamasisha na kuimarisha malezi bora, pamoja na kuongeza uelewa kwa jamii juu ya haki na ustawi wa mtoto.

Awali Meneja Programu wa taasisi ya SOS Children’s Village mkoa wa Arusha, Mpely Ally Kalonge, amesema kuwa lengo la shirika hilo ni kutoa malezi mbadala kwa watoto wanaohitaji msaada, pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto na kupinga vitendo vya ukatili katika jamii.

Amesema taasisi ya SOS Children village imekuwa kiunganishi Kikubwa kati yake na jamii kwa kusaidia kuanzisha makundi ya malezi katika Halmashauri nne ndani ya Mkoa wa Arusha sanjari na kuyapatia  elimu ya malezi na makuzi makundi hayo.

Kalonge amesema mpango wa taasisi ni kuendelea kuongeza makundi hayo Ili kuongeza ustawi na ulinzi wa watoto na kujenga jamii yenye upendo na isiyo na matendo ya kikatili.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...