
Farida Mangube, Morogoro
CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeandaa hafla ya Iftar kwa watumishi wake waumini wa Dini ya Kiislamu ikiwa ni sehemu ya kuimarisha umoja, mshikamano na mahusiano mema miongoni mwa wanajumuiya wa chuo.
Hafla hiyo imefanyika Machi 13, 2026 katika Ukumbi wa Multipurpose uliopo Kampasi ya Edward Moringe, na kuhudhuriwa na watumishi mbalimbali wa chuo waliokusanyika pamoja kushiriki futari katika mazingira ya upendo na ushirikiano.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Raphael Chibunda, amesema tukio hilo ni sehemu ya juhudi za chuo kuendelea kujenga utamaduni wa kuheshimiana, kushirikiana na kuimarisha mshikamano miongoni mwa watumishi wake bila kujali tofauti za kiimani.
Amesema SUA inaamini kuwa matukio ya kijamii na kiimani kama hayo huchangia kuimarisha uhusiano mzuri kazini na kujenga mazingira bora ya kazi yanayochochea maendeleo ya taasisi.
Baadhi ya watumishi walioshiriki katika hafla hiyo wameeleza kufurahishwa na utaratibu huo, wakisema unaleta pamoja wanajumuiya wa chuo na kuimarisha mshikamano, hususan katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kupitia hafla hiyo, SUA imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kujenga jamii ya chuo inayothamini umoja, mshikamano na kuheshimiana, sambamba na kuendeleza maadili mema yanayochangia ustawi wa wanajumuiya wake na maendeleo ya taasisi kwa ujumla.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...