Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, limepanda zaidi ya miche ya miti elfu mbili ya vivuli pamoja na miche 420 ya matunda katika eneo lenye ukubwa wa heka tisa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono kampeni ya uhifadhi wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza Machi 27, 2026 wakati wa zoezi la upandaji miti,  lililofanyika katika eneo la ofisi za TANESCO wilayani humo, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Janeth Mayanja, amelipongeza shirika hilo kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha upandaji miti kupitia kauli mbiu ya “Nitunze Nikutunze”.

Amesema wilaya hiyo imejiwekea lengo la kupanda miti laki mbili  katika kipindi hiki cha masika, ambapo miche tayari ipo katika vitalu vya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilayani humo.

Aidha, amesema katika vijiji vyote 107 vya wilaya hiyo, miche ya miti elfu moja imegawiwa kwa kila kijiji na wananchi wamepewa bure ili kuipanda katika makazi yao na mashamba, hatua inayolenga kuongeza uoto wa asili na kuboresha mazingira.

Mhe. Mayanja ameongeza kuwa ndani ya miaka mitatu, eneo hilo linatarajiwa kuwa na miti mingi itakayosaidia kutoa kivuli, matunda pamoja na hewa safi kwa wananchi wanaofika kupata huduma mbalimbali kwenye ofisi hiyo.

Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Chamwino, Mhandisi Judith Beatus, amesema zoezi hilo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira.

Naye mwakilishi wa Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, James Vesso, amesema lengo la kupanda miti hiyo ni kuboresha mandhari ya Jiji la Dodoma na kuongeza kuwa shirika hilo limejipanga kuhakikisha miti yote iliyopandwa inalindwa na kukua vizuri.

Kipekee amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, kuwezesha zoezi hilo kwa kutenga rasilimali fedha, huku akisisitiza kuwa juhudi za upandaji miti zitaendelea kuwa endelevu ndani ya shirika hilo.

Kwa ujumla, juhudi hizi zinaonesha dhamira ya dhati ya TANESCO na Serikali katika kulinda mazingira, huku wananchi wakihimizwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika upandaji na utunzaji wa miti kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.







 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...