Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ruvuma, Alan Njiro amewahimiza wananchi kujikita katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia majiko ya umeme ya kisasa, akibainisha kuwa hatua hiyo ni salama, nafuu na rafiki kwa mazingira.

Akizungumza Machi 20, 2026 wakati akiwasilisha mada kuhusu nishati safi ya kupikia katika mafunzo ya ndani ya watumishi wa Shirika la ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika COASCO, yaliyolenga kuwajengea uwezo katika masuala ya utumishi wa umma, rushwa, afya ya akili na UKIMWI.

Njiro amesema kuwa TANESCO imefanya tafiti juu ya matumizi ya majiko ya umeme ikiwemo induction cooker na pressure cooker, na kubaini kuwa vifaa hivyo vinatumia umeme kidogo (energy saver) na vinafaa kwa matumizi ya kila siku majumbani.

Alieleza kuwa tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo wananchi walikuwa na hofu ya gharama kubwa za umeme, teknolojia ya sasa imeboreshwa na kufanya majiko ya umeme kuwa na matumizi madogo ya nishati. Aidha, aliwataka wananchi kuepuka kutumia vifaa vya mtumba ambavyo mara nyingi hutumia umeme mwingi na kuongeza gharama zisizo za lazima.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano Msaidizi wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma, Emma Ulendo alisema majiko ya induction cooker ni salama zaidi kwani hutumia mfumo wa sumaku kati ya sufuria na jiko, hivyo kupunguza hatari ya mtumiaji kupigwa na shoti au kusababisha ajali za moto. Aliongeza kuwa majiko hayo yana uwezo wa kuweka muda wa kupika na kujizima yenyewe, jambo linalosaidia kuokoa umeme na kuongeza usalama kwa mtumiaji.

Ulendo pia alisisitiza kuwa matumizi ya pressure cooker yana mchango mkubwa katika kupunguza muda wa kupika na hivyo kutumia umeme kidogo, hali inayofanya majiko hayo kuwa suluhisho bora kwa kaya nyingi zinazotaka kupunguza gharama na kulinda mazingira.

Katika hatua nyingine, Njiro alibainisha kuwa Mkoa wa Ruvuma una umeme wa kutosha, ukiwa na matumizi  ya takribani megawati 28 huku ukisalia  na ziada ya megawati 42, hali inayowezesha wananchi kutumia umeme huo kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kupikia bila hofu ya upungufu wa nishati hiyo muhimu.

Kwa ujumla, TANESCO imeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia umeme, hatua ambayo itasaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kulinda mazingira na kuboresha afya pamoja na maisha ya wananchi kwa ujumla.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...