Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza kufurahishwa na ushirikiano wa kimatibabu kati ya Hospitali ya Benjamin Mkapa na Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna, huku ikikaribisha upanuzi wa ushirikiano huo katika taasisi nyingine za kibobezi ikiwemo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), kwa lengo la kuboresha huduma za afya nchini.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya nje, Mhe. Ngwaru Maghembe (Mb), akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), katika mazungumzo ya kidiplomasia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria anayeshughulikia masuala ya kisiasa, Mhe. Balozi Dkt. Hannah Liko, yaliyofanyika Machi 24, 2026 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Maghembe amepongeza mchango wa Austria katika sekta ya elimu, ikiwemo utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu na utekelezaji wa miradi ya kujifunza kwa njia ya mtandao (e-learning) visiwani Zanzibar kupitia kampuni ya eeeAustria GmbH. Ameiomba Austria kuongeza nafasi za masomo ya uzamili na uzamivu kwa Watanzania, hususan katika nyanja za Teknolojia ya Habari, kilimo na utalii.

Aidha, amekaribisha mpango wa Global Gateway wa Umoja wa Ulaya (EU) kama nyenzo muhimu ya kuhamisha ushirikiano kutoka misaada ya jadi kuelekea uwekezaji wa kimkakati na biashara. Pia ameeleza azma ya kuandaa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji katika robo ya pili ya mwaka 2026 ili kutangaza fursa zilizopo chini ya Dira ya Maendeleo ya 2050.

Kwa upande wake, Dkt. Liko amesisitiza utayari wa Austria kuendelea kushirikiana na Tanzania licha ya changamoto za siasa za kimataifa. Amesema Austria itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta ya utalii kupitia kubadilishana uzoefu na wataalamu, pamoja na kuonesha nia ya kusaidia miradi mbalimbali ikiwemo ya nishati.

Katika mazungumzo hayo Tanzania imeihimiza Austria kufungua ubalozi mkazi nchini ili kurahisisha uratibu wa miradi ya maendeleo.














Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...