SERIKALI ya Tanzania na Chuo Kikuu cha Limerick cha nchini Ireland wamesaini hati ya makubaliano ya utekelezaji wa ufadhili wa Samia Scholarship Extended, utakaosomesha wanafunzi 32 kwenye chuo hicho.
Makubaliano hayo yamefanyika leo Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda pamoja na ujumbe kutoka ubalozi wa Ireland nchini Tanzania na kutoka chuo cha Limerick.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa hati hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa ufadhili huo ni sehemu ya ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa mwaka jana wakati wa kuzindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuimarisha elimu nchini kwa kuzalisha wataalamu watakaosomea sayansi na teknolojia ili kuendana na matakwa ya dunia.
Amesema ushirikiano huo umekuja wakati muafaka, wakati Tanzania ikiendelea kuwekeza katika uchumi unaotegemea maarifa na ubunifu.
Pia alisema unaonesha dhamira ya pamoja ya kuwawezesha vijana kupitia elimu bora, uzoefu wa kimataifa na ujuzi wa kisasa kwa ajili ya baadaye, kwani chuo hicho kinatoa punguzo la ada kwa asilimia 50 kwa wanafunzi.
Alisema Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Samia Scholarship katika Sayansi ya Data, Akili Unde (AI) na taaluma zinazohusiana na mpango wa kimkakati unaolenga kuwajengea vijana maarifa na ujuzi katika teknolojia mpya.
“Tumewapeleka wanafunzi 34 waliofanya vizuri kwenye mitihani yao ya kidato cha sita nchini Ireland ambapo wanafunzi 32 wamepata ufadhili kwenye chuo kikuu cha Limerick, chuo kinachoongoza kwa teknolojia na mafunzo ya vitendo, na wengine wawili tumewapeleka kwenye chuo cha Cork nchini Ireland,” amesema Profesa Mkenda.
Prof. Mkenda amesema kuwa wanafunzi hao ni sehemu ya ufadhili wa ‘Samia Scholarship’ kwa wanafunzi 50 waliofanya vizuri kwenye mitihani ya kidato cha sita ambapo tayari wanafunzi 16 wameshajiunga na chuo kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Prof. Mkenda amesema kuwa wizara hiyo inatekeleza agizo la Rais Samia kwa vitendo, “Mwaka huu tutawapeleka wanafunzi 50 katika vyuo vikuu mbalimbali vya nje, mwakani tutafanya zaidi.”
Waziri Mkenda amesema kuwa fursa hiyo inafungua mlango kwa watoto wa masikini kusoma kwenye vyuo vikuu vya nje bure. “Sisi Serikali tunagharamia nauli za kwenda na kurejea katika nchi husika na vyuo vinawasomesha bure. Hii fursa itawasaidia watoto wa wakulima, wafugaji au hata wamachinga.”
Kwa upande wake, Balozi wa Ireland nchini, Nicola Brennan amehimiza Serikali kuzingatia maono ya maendeleo ya muda mrefu, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na 2050 kwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu bora ili vijana waweze kupata ajira na kuchangia katika maendeleo ya nchi.
Alisema Tanzania ina msingi mzuri wa rasilimali watu, utulivu wa nchi unaendelea kuimarika na idadi kubwa ya vijana huku kukiwa na fursa kubwa ya kukuza uwezo wao.
“Ifikapo mwaka 2050, idadi ya watu Tanzania inatarajiwa kuongezeka maradufu kutoka takribani milioni 67 hadi zaidi ya milioni 130. Hili ni changamoto kubwa kuhakikisha vijana wanapata ajira,” alisema Nicola.
Aliongeza kuwa ni muhimu kuhakikisha vijana wanapata elimu bora na ujuzi unaowawezesha kupata ajira na kuchangia katika maendeleo ya nchi, akisisitiza elimu ni jambo la msingi sana.
Alisema kwa Ireland, uwekezaji katika elimu ni moja ya sababu kubwa zilizoifanya kufikia mafanikio makubwa kiuchumi, ukuaji na maendeleo na kuifanya kuwa ni nchi iliyoelimika zaidi duniani.
Alihimiza Serikali kuzingatia maono ya maendeleo ya muda mrefu, ikiwemo Dira 2050, kwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu bora ili vijana waweze kupata ajira na kuchangia katika maendeleo ya nchi.
Alisema kuwa Chuo Kikuu cha Limerick ni chuo chenye kufundisha sayansi na teknolojia inayoendana na mahitaji ya wakati.
“Kwa sasa dunia ipo kwenye uvumbuzi wa kisayansi na teknolojia mpya ikiwa pamoja na akili unde (Artificial Intelligence).”
Naye, Profesa Colin Fitzpatrick, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Limerick amesema kuwa chuo hicho kinasifika katika ufundishaji wa vitendo pamoja na kuwapeleka wanafunzi wake kwenye kampuni zilizofanikiwa duniani ili kuongeza uzoefu na kuona uhalisia wa kile walichojifunza.
Amesema kuwa Ireland ni taifa linaloongoza kwa kuwa na kampuni kubwa za kiteknolojia barani Ulaya, hivyo anatarajia wanafunzi hao kutoka Tanzania watapata tija ya kujifunza nadharia na vitendo.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...