NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuhamasisha wafanyabiashara wanawake kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili kukidhi matakwa ya sheria za viwango, wakati wa Maonesho ya Miaka 20 ya Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa TBS Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Noor Meghji, amesema ushiriki wa shirika hilo unalenga kutoa elimu kwa wafanyabiashara wanawake, hususan wajasiriamali wadogo, ambao bado hawajathibitisha ubora wa bidhaa zao.

Amesema TBS ni mdau muhimu wa wafanyabiashara na ipo tayari kuwawezesha kufikia viwango vinavyotakiwa kisheria ili kuhakikisha bidhaa wanazozalisha zinakuwa na ubora unaokubalika sokoni.

“Tupo hapa kuhamasisha wafanyabiashara hawa waweze kukidhi vigezo vya ubora wa bidhaa zao. Tunatambua kuwa wengi wao ni wajasiriamali wadogo na wanahitaji msaada wa kitaalamu ili kufikia viwango,” amesema Meghji.

Alifafanua kuwa TBS ina programu maalumu ya kuwawezesha wafanyabiashara wanawake, hasa waliopo katika sekta ya viwanda, kwa kuwasaidia kufikia vigezo vya uthibitishaji wa ubora bila gharama.

“Tunafahamu kuna wazalishaji wengi wadogo wanawake hawana uwezo wa kumudu gharama za kuthibitisha ubora wa bidhaa zao. Kwa hiyo, tuna programu ya kuthibitisha ubora bure kwa gharama za Serikali,” ameeleza.

Kwa mujibu wa Meghji, sharti la msingi kwa mjasiriamali ni kuwa na barua ya utambulisho kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), kisha kuwasilisha maombi TBS ambapo mchakato wa uthibitishaji huanza mara moja.

Amesisitiza kuwa hakuna sababu kwa mfanyabiashara yeyote, akiwemo mwanamke, kushindwa kukidhi viwango, akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kulinda afya na usalama wa watumiaji pamoja na kupanua soko la bidhaa zao.

Kwa upande wake, mfanyabiashara Lily Mwaigomole ameishukuru TBS kwa elimu waliyoitoa, akisema imefungua uelewa wake kuhusu umuhimu wa Nembo ya Ubora ya TBS katika kukuza biashara.

“Nimefurahi kuona maofisa wa TBS wakipita kwenye mabanda wakitoa elimu kuhusu umuhimu wa kukidhi matakwa ya viwango. Mimi bado sina Nembo ya Ubora, lakini nitaanza mchakato wa kuipata ili niweze kupanua soko na kuongeza imani kwa wateja,” amesema.

Maonesho hayo ya kuadhimisha miaka 20 ya TWCC yalianza Februari 26 na kuhitimishwa Machi 2 mwaka huu, yakilenga kuwaunganisha wafanyabiashara wanawake na wadau mbalimbali wa maendeleo.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...