Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Kituo cha Hali ya Hewa cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), imeadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa kutoa elimu kwa wadau pamoja na kuweka mipango ya kuendelea kutoa huduma bora, kuongeza tija na ufanisi, na kuhakikisha usalama wa usafiri wa anga kwa kutoa taarifa sahihi.

Akizungumza leo, Machi 23, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi waliotembelea Kituo cha Hali ya Hewa cha JNIA, Meneja wa TMA wa Huduma za Hali ya Hewa katika Usafiri wa Anga na Msimamizi wa Kituo cha Hali ya Hewa JNIA, John Mayunga, amesema kuwa ni muhimu kuelimisha jamii ili iweze kuchukua tahadhari na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mayunga ameongeza kuwa kuna mchango mkubwa wa utoaji wa tahadhari mapema kabla jamii haijakumbwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, kwani majanga mengi duniani yamehusishwa na hali mbaya ya hewa.

“Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa wa kimkakati katika huduma za hali ya hewa kwa kununua vifaa vya kisasa pamoja na kuajiri wataalamu, jambo ambalo limesaidia kupata taarifa sahihi za hali ya hewa kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya wadau na kijamii,” amesema Mayunga.

Aidha, Mayunga amesisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo vijana kwa kuzingatia umuhimu wa taarifa za hali ya hewa, kwani wao ni taifa la kesho, huku akifafanua kuwa TMA ni miongoni mwa taasisi za kwanza barani Afrika kupata cheti cha ubora katika huduma za hali ya hewa kwa usafiri wa anga.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Kituo cha Uangazi TMA–JNIA, Ally Selemani, amesema wanajivunia kutumia teknolojia ya kisasa iliyowawezesha kutoa taarifa za uhakika za hali ya hewa na kupunguza changamoto kwa kiwango kikubwa katika utendaji wa kazi.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi, Shaneli Kaguli na Isabela Dany kutoka Shule ya Msingi Daddy, wameishukuru TMA kwa kuwaelimisha kuhusu utendaji wa kazi zao, jambo linalowasaidia kuwa na uelewa zaidi kuhusu matumizi ya taarifa za hali ya hewa na namna ya kukabiliana na athari zinazoweza kutokea.

Maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani 2026 yamebeba kaulimbiu isemayo: “Pima hali ya hewa leo, ili kesho iwe salama”





Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...