Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kuelekea maadhimisho ya miaka 25 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Mkurugenzi wa chuo hicho Kampasi ya Dar es Salaam, Mussa Lugembe, amewataka wanafunzi wa vyuo na shule za sekondari kuwa waadilifu na wazalendo ili kujenga msingi imara wa utumishi wa umma wenye uwajibikaji nchini.
Lugembe alitoa wito huo alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Azania jijini Dar es Salaam, ambapo alisema chuo hicho kimeanza kutoa elimu ya maadili na uzalendo kwa vijana ili kuwajengea uelewa mapema kuhusu misingi ya utumishi wa umma kabla hawajaingia rasmi katika ajira za serikali.
Alieleza kuwa lengo la mpango huo ni kuwaandaa watumishi wa umma wa baadaye wanaotambua wajibu wao kwa taifa, wanaozingatia maadili ya kazi, uwajibikaji na uzalendo wanapokuwa katika nafasi mbalimbali za utumishi wa umma.
“Tunataka vijana waanze kujifunza mapema kuhusu maadili ya utumishi wa umma ili wanapopata nafasi za ajira wawe tayari kulitumikia taifa kwa uadilifu, uwajibikaji na uzalendo,” alisema Lugembe.
Naye mwanafunzi wa Azania, Faidh Mussa, alisema elimu hiyo imewasaidia wanafunzi kuelewa umuhimu wa uzalendo, uwajibikaji na maadili katika kujenga taifa lenye maendeleo.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Mwishehe Ming’uno, alisema mafunzo hayo yanawapa motisha wanafunzi kuzingatia maadili ya kazi na kujiandaa kuwa watumishi wa umma watakaolitumikia taifa kwa ufanisi na uadilifu.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...