Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP Tanzania) kwa kushirikiana na Serikali ya Uingereza kupitia Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO), wametoa zaidi ya Shilingi milioni 70 kama mtaji wa awali kwa biashara bunifu zilizoanzishwa na wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.

Msaada huo umetolewa katika msimu wa pili wa Mpango wa Kubadilishana Ujuzi miongoni mwa wahadhiri wa vyuo vikuu Afrika Mashariki, uliofanyika kwa siku tatu katika Chuo cha Indian Institute of Technology Madras (IIT Madras) kampasi ya Zanzibar.

Mpango huo uliwakutanisha wanafunzi wabunifu, viongozi wa vyuo vikuu, wakufunzi na wadau wa mfumo wa ubunifu kwa lengo la kuimarisha nafasi ya vyuo vikuu kama chachu ya ujasiriamali na ubunifu.

Programu hiyo inaendeleza mafanikio ya toleo la kwanza lililojulikana kama RISE 4.0, ambalo limekuwa likiwasaidia wabunifu vijana kubadilisha mawazo yao kutoka vyuoni na kuyageuza kuwa biashara halisi zinazoweza kukua.

Mpango huo unatekelezwa na UNDP kupitia Mradi wa FUNGUO kwa ushirikiano na Serikali ya Uingereza kupitia FCDO. Ushirikiano huo unalenga kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini kwa kuwaunganisha wanafunzi na ushauri elekezi, fursa za ufadhili pamoja na mazingira yatakayosaidia mawazo yao kukua na kuwa biashara endelevu.

Kabla ya kutangazwa kwa washindi, timu za wanafunzi zilipata mafunzo na ushauri kutoka kwa wataalamu wa vyuo vikuu shiriki pamoja na wadau wa mfumo wa ubunifu.

Mafunzo hayo yalihusu uundaji wa mawazo ya biashara, kukuza biashara changa, mikakati ya kuingiza ubunifu sokoni na namna ya kujenga biashara zinazoweza kupanuka na kushindana sokoni.

Jumla ya biashara bunifu sita ziliingia fainali za mwaka huu ambazo ni Vestis, Naarad, CropIQ, Carbon Trace, Ecofy na Power Taka.

Mshindi wa jumla, Vestis, biashara iliyoanzishwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ilipokea Shilingi milioni 15 kama mtaji wa awali. Jukwaa hilo la kidijitali linalenga kurahisisha ununuzi na uuzaji wa nguo mtandaoni na kuwasaidia watumiaji kuokoa muda na gharama za usafiri.

Mbali na mtaji huo wa awali, biashara hizo bunifu pia zitapata msaada endelevu ikiwemo fursa za kuwasilisha mawazo yao kwa wawekezaji, mafunzo ya masoko na uendeshaji wa biashara, ushauri elekezi pamoja na fursa za kujenga mitandao na wadau wa ubunifu na wawekezaji watarajiwa.

Akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo, Meneja wa Mpango wa FUNGUO wa UNDP Tanzania, Joseph Manirakiza, alisema toleo la pili la mpango huo linaonyesha dhamira ya UNDP katika kukuza ubunifu kwa vijana nchini.

Alisema kupitia mpango huo, zaidi ya biashara bunifu 70 zinazoongozwa na wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali tayari zimenufaika.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uendelezaji na Uhawilishaji wa Teknolojia (COSTECH), Dkt. Erasto Mlyuka, alisema serikali inaunga mkono programu zinazochochea ubunifu na ujasiriamali kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Alisema vyuo vikuu vinapaswa kuwajengea wanafunzi ujuzi wa ujasiriamali ili wanapohitimu wawe tayari kuanzisha biashara zao badala ya kutegemea ajira pekee.

Akizungumza kwa niaba ya timu iliyoshinda, mwakilishi wa kampuni ya Vestis, Kelvin Erasto, alisema fedha hizo zitasaidia kupanua jukwaa la biashara hiyo na kuwafikia watumiaji wengi zaidi.




Alisema pia wanatarajia kuendelea kupata mafunzo na ushauri kutoka kwa wataalamu wa vyuo vikuu ili kuimarisha mtindo wao wa biashara na kuharakisha ukuaji wake.

Mpango huo umefanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Vyuo Vikuu kama Injini za Ubunifu: Kujenga Njia Endelevu kutoka Maarifa mpaka Biashara.”

Katika mkutano huo wa siku tatu uliofanyika kuanzia Machi 4 hadi 6, wahadhiri wa vyuo vikuu, watunga sera na wadau wa ubunifu walijadili namna taasisi za elimu ya juu zinavyoweza kuchochea zaidi uanzishaji wa biashara bunifu, uendelezaji wa tafiti zenye tija kibiashara na ukuaji wa biashara zinazoendeshwa kwa ubunifu nchini Tanzania na Afrika Mashariki.



Kupitia ujenzi wa uwezo, ushauri elekezi na mtaji wa awali, mpango huo unalenga kuimarisha biashara bunifu zinazozaliwa vyuoni ambazo zina uwezo wa kuzalisha ajira, kutatua changamoto za maendeleo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa ubunifu nchini.



























Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...