Watanzania wameendelea kutoa ushindani wa kiwango cha juu katika mbio za kilomita 21 zinazobebwa na tamasha kubwa la kila mwaka la Kili International Marathon ambalo pia ni moja ya matukio makubwa ya kimichezo barani Afrika.

Kupitia matokea ya mbio hizo, kategori ya wanaume iliongozwa na Bw. Michael Geay aliyetwaa dhahabu baada ya kukimbia kwa 1:04:10, akifuatwa kwa karibu na Josephat Joshua Gisumo aliyemaliza kwa 1:04:14, huku mkimbiaji wa Kenya, James Kairiuki, akishika nafasi ya tatu kwa 1:04:30. Kwa upande wa wanawake, Hamida Musa aliongoza safu ya Watanzania, akifuatiwa na Failuna Matanga, huku Mkenya Veronika Wanjiku akimaliza wa tatu.

Akizungumza mara baada ya kukamilisha mbio, Geay alisema ushindani ulikuwa mkali lakini akasisitiza fahari yake ya kuiwakilisha nchi. Alieleza kuwa, “Nimefurahi sana kushinda. Haikuwa rahisi, kwani kila mmoja alikuwa analenga medali ya dhahabu.”

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, aliwapongeza wanariadha kwa nidhamu, uzalendo na uthabiti wao. Alisoma pia salamu za pongezi kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameahidi kuwa mgeni rasmi katika mbio za mwakani na kuongeza zawadi ya washindi kwa shilingi milioni 100.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas, Pierre Canton Bacara, alieleza kuwa kiwango cha ushindani kimeendelea kupanda na kusisitiza dhamira ya kampuni kuendeleza michezo, kuimarisha uhusiano na jamii na kuendeleza miradi ya mazingira, ikiwemo upandaji wa miti zaidi ya 50,000 katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro.

Bacara amesisitiza kuhusu kaulimbiu ya mwaka huu ya “Kila Kona, Kila Hatua Kasi zaidi,” kuwa inaakisi juhudi za kampuni kuhakikisha huduma za mawasiliano ya 4G na 5G zinawafikia Watanzania kote nchini.

Aliongeza kuwa, “Kwa mwaka wa tatu mfululizo, Kampuni hiyo imetambuliwa kimataifa na Ookla kama mtandao wenye kasi zaidi nchini. “Tunaendelea kuwekeza katika miundombinu ili kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na mawasiliano ya uhakika-iwe ni biashara, elimu, kilimo au kusherehekea mafanikio ya ushindi wa mbio kama hizi za Yas Kili International Half Marathon mtandaoni.”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, aliipongeza Yas kwa kuendeleza urafiki wa muda mrefu na jamii ya mkoa huo na kusema mbio hizo zimekuwa kichocheo cha utalii, biashara na maendeleo ya jamii.

Katika mbio za Yas Kili Half Marathon kwa mwaka huu, maelfu ya Watanzania wamejitokeza kushiriki huku viwango vya ushindani vikipanda, na ushindi katika makundi mbalimbali ukitawaliwa na wanariadha wa ndani, jambo lililoleta hamasa kubwa miongoni mwa mashabiki.

Mbio za Yas Kili International Marathon kwa mwaka 2026 zimevutia umati mkubwa wa washiriki na watazamaji, likidhihirisha ukubwa wa mbio hizi katika kukuza uzalendo, kuhamasisha utalii na kuonesha hadhi ya Tanzania inavyozidi kuimarika katika mbio za masafa marefu.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...