📍Awataka viongozi wa dini kuhubiri Umoja na mshikamano

NA MWANDISHI WETU, MBEYA

MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, ametoa wito kwa viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kuimarisha vita dhidi ya mmomonyoko wa maadili, huku akisisitiza kuwa wanawake ni nguzo muhimu katika kulea kizazi chenye nidhamu na uzalendo nchini.

Mhe. Itunda ametoa kauli hiyo Jumamosi, Februari 28, 2026, alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, katika ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Wanawake wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) lililofanyika katika ukumbi wa VETA jijini Mbeya.

Akihutubia washiriki wa kongamano hilo waliotoka katika mikoa zaidi ya 13 nchini, DC Itunda alisema Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango wa kipekee wa wanawake katika kulinda misingi ya amani, maadili na hofu ya Mungu, mambo ambayo ni chemchemi ya ustawi wa Taifa.

"Wanawake ni nguzo ya Taifa. Serikali inaendelea kuthamini ushirikiano na taasisi za kidini katika kukuza maadili na kuchochea maendeleo. Ni wajibu wenu kuendelea kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa kusimamia malezi na kupinga kwa nguvu zote vitendo vinavyovunja heshima ya jamii yetu," alisisitiza Mhe. Itunda.

Pia aliwataka viongozi wa dini pamoja na kusimamia mmomonyoko wa maadili lakini pia amewaasa kuhakikisha wanahubiri amani ya nchi, upendo na mshikamano na kuwaunga mkono viongozi nchini.

Asifu Falsafa ya 4R ya Rais Samia

Katika hatua nyingine, Mhe. Itunda alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake uliotukuka unaopambanuliwa na falsafa ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Mpya).

Alibainisha kuwa kupitia falsafa hiyo, Rais Samia amefanikiwa kuliunganisha Taifa, kuimarisha maridhiano kati ya makundi mbalimbali na kujenga mazingira ya amani yanayowezesha mikutano mikubwa kama hiyo ya CCT kufanyika kwa utulivu.

"Falsafa ya 4R imekuwa dira yetu katika kujenga mshikamano wa kitaifa na kuvumiliana. Mkoa wa Mbeya utaendelea kuwa kitovu cha makongamano yenye tija kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Serikali na taasisi za kidini," alisema.

Viongozi wa Dini Waimwagia Sifa Serikali

Kwa upande wao, viongozi wa dini waliohudhuria kongamano hilo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki ya kuabudu na kufanya shughuli za kijamii.

Kongamano hilo limehitimishwa kwa maombi maalum ya kuliombea Taifa, viongozi wa Serikali na kuliombea Kanisa ili liendelee kuwa nuru ya maadili nchini.

Viongozi waliohudhuria ni pamoja na Askofu wa Dayosisi ya Konde (KKKT), Baba Askofu Gefrey Mwaihaba, Katibu Mkuu wa CCT, Mchungaji Canon Dkt. Moses Matonya, pamoja na Maaskofu wa Makanisa ya Anglikana na Moravian (Jimbo la Mbeya).







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...