Wanawake wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) wameungana na wanawake wengine kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani 2026, katika maadhimisho ya kimkoa yaliyofanyika Machi 8, 2026 katika Viwanja vya Barafu Mburahati, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wanawake kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mhe. Chalamila aliwahimiza wanawake kuendelea kutumia fursa zilizopo ili kujiendeleza kiuchumi na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Alisema wanawake wana nafasi kubwa katika maendeleo ya jamii na taifa, hivyo ni muhimu waendelee kupewa na kutumia kikamilifu fursa zilizopo kwa ajili ya kufikia maendeleo jumuishi.
“Wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii na taifa, hivyo ni muhimu waendelee kupewa na kutumia kikamilifu fursa zilizopo ili kufikia maendeleo jumuishi,” alisema Chalamila.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake TUICO tawi la NBAA Bi. Irene Mutagaywa amesema kuwa kaulimbiu ya maadhimisho hayo ambayo ni “Haki na usawa kwa wanawake na wasichana,” inalenga kuhamasisha jamii kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki na fursa sawa katika nyanja mbalimbali za maisha, jambo ambalo pia linaendana na malengo ya maendeleo ya kimataifa kuelekea mwaka 2030 na ajenda ya maendeleo ya mwaka 2050.
Pia amesema maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wanawake kutoka sekta mbalimbali kujadili masuala ya usawa wa kijinsia, haki za wanawake pamoja na mchango wao katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi, ikiwa ni siku maalum ya kutambua mchango wa wanawake katika jamii na kuendelea kuhamasisha usawa wa kijinsia.
Historia ya siku hiyo inaanzia mwaka 1908, ambapo wanawake takribani 15,000 waliandamana katika mji wa New York, Marekani, wakidai kupunguziwa muda wa kazi, ujira wa kuridhisha na haki ya kupiga kura. Mwaka uliofuata, chama cha kisoshalisti cha Amerika kilitangaza siku ya kwanza ya kitaifa ya wanawake.
Wazo la kuifanya kuwa Siku ya Wanawake Kimataifa lilianzishwa mwaka 1910 na mwanaharakati wa haki za wanawake Clara Zetkin, wakati wa mkutano wa kimataifa wa wafanyakazi wanawake uliofanyika Copenhagen, Denmark.
Picha mbalimbali za matukio ya wafanyakazi wanawake wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) katika maadhimisho ya Siku ya wanawake Kimataifa yaliyofanyika Machi 08, 2025 katikaViwanja vya Barafu Mburahati, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila pamoja na viongozi mbalimbali wakiwapungia mikono wafanyakazi wanawake wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) katika maadhimisho ya Siku ya wanawake Kimataifa.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...