
TUME ya Ushindani (FCC) kupitia Kanda ya Ziwa imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kutoa elimu ya ulinzi wa mlaji kupitia Kliniki ya Mlaji inayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mkendo, Manispaa ya Musoma.
Katika kuimarisha uelewa wa wadau mbalimbali, FCC haikuishia kwa wananchi pekee bali pia ilifanya ziara maalum kwa baadhi ya taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha katika manispaa hiyo, kwa lengo la kuzielimisha juu ya wajibu wao wa kuzingatia sheria na kanuni katika utoaji wa huduma.
Akiongoza zoezi hilo, Mkuu wa Kanda ya Ziwa,Bw. Frank Mdimi, akishirikiana na Afisa Biashara wa Manispaa ya Musoma, Joshua Mlole pamoja na maafisa wengine, walitembelea taasisi za Enokwe, Pongeza na Ohura na kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na watoa huduma hao.
Katika ziara hiyo, maafisa wa FCC wamesisitiza umuhimu wa kuandaa mikataba ya huduma kwa uwazi na haki, wakielekeza taasisi hizo kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ushindani inasimamia na kudhibiti Mikataba ya Mlaji inayoandaliwa na watoa huduma
Watoa huduma kutoka taasisi hizo walionesha utayari mkubwa wa kupokea maelekezo hayo, wakieleza kufurahishwa kwao na hatua ya FCC kuwafuata na kuwapatia elimu kwa vitendo. Wamesisitiza kuwa elimu hiyo itawasaidia kuboresha huduma zao na kujenga uaminifu kwa wateja wao.
Aidha, taasisi hizo zimeahidi kushirikiana kwa karibu na FCC kwa kuhakikisha zinazingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali, pamoja na kudumisha mawasiliano ya mara kwa mara ili kuboresha zaidi sekta ya huduma ndogo za fedha.
Zoezi la utoaji elimu kupitia Kliniki ya Mlaji linaendelea Machi 27, ambapo wananchi wataendelea kupatiwa elimu kuhusu haki zao, wajibu wao na namna bora ya kujilinda wanapotumia huduma mbalimbali sokoni.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...