Na Farida Mangube, Morogoro
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, ameagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuandaa mpango madhubuti wa kuwawezesha wananchi kuzalisha nishati safi ya kupikia kwa kutumia pumba za mpunga.
Agizo hilo limetolewa wakati wa ufunguzi wa kongamano la kitaifa la nishati safi lililofanyika mkoani Morogoro, likihusisha wadau kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Hatua hiyo inalenga kupunguza gharama za nishati, kulinda misitu na kuboresha afya za wananchi wanaotegemea kuni na mkaa wa miti.
Serikali pia imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye mitungi ya gesi na mashine za kuchakata mkaa mbadala, hatua inayotarajiwa kurahisisha upatikanaji wa nishati safi na kupunguza gharama kwa watumiaji na wazalishaji.
Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri Ndejembi amesema uwezeshaji wa wananchi utasaidia kuhamasisha uhamaji kutoka matumizi ya nishati chafu kwenda kwenye nishati endelevu, huku pia ukichangia ukuaji wa uchumi wa familia na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa UONGOZI Institute, Kadiri Singo, amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ni njia muhimu ya kupunguza madhara ya kiafya, kulinda mazingira na kukuza uchumi wa taifa.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Kighoma Malima, amesema mkoa umeanza kutoza ushuru wa shilingi 20,000 kwa kila gunia la mkaa wa miti ili kudhibiti ukataji holela wa miti, huku uwekezaji katika teknolojia ya kuchakata pumba za mpunga ukitarajiwa kufungua ajira na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.
Kampeni ya kitaifa ya elimu kuhusu faida za nishati safi tayari imeanza katika mikoa ya Tanga, Dodoma, Morogoro na Njombe, huku mpango huo ukiwa na lengo la kufikia wananchi wote nchini.



.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...