Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Gladness Kirei, ametoa wito kwa jamii pamoja na mashirika mbalimbali nchini kuwasaidia wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito, ili waweze kurejea katika mfumo rasmi wa elimu na kukabiliana na changamoto wanazokumbana nazo, hususan unyanyapaa.

Dkt. Kirei alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kukabiliana na unyanyapaa kwa wanafunzi wanaorejea shuleni, iliyoandaliwa na Taasisi ya Msichana Initiative.

Alisema hatua hiyo imechukuliwa kufuatia kubainika kuwa baadhi ya wanafunzi waliorejea shuleni kwa mujibu wa Waraka wa Elimu Na. 2 wa mwaka 2021 wamekuwa wakiacha tena masomo kutokana na unyanyapaa kutoka kwa jamii, walimu na wanafunzi wenzao.

“Wapo wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo kutokana na mazingira yasiyo rafiki yanayotokana na unyanyapaa. Muongozo unaeleza wazi kuwa mwanafunzi ana haki ya kuhamia shule nyingine endapo atakumbana na hali hiyo,” alisema Dkt. Kirei.

Aidha, aliipongeza Taasisi ya Msichana Initiative kwa juhudi zake za kupigania haki za wasichana, akieleza kuwa kampeni hiyo itasaidia kuhamasisha jamii kuwatambua wanafunzi hao kama wengine na kuwaunga mkono ili wafikie ndoto zao.

Alisisitiza umuhimu wa kuwasaidia wanafunzi hao kwa kuwapatia mahitaji muhimu ikiwemo vifaa vya shule pamoja na msaada wa kisaikolojia ili waweze kuendelea na masomo kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Msichana Initiative, Consolata Chikoti, alisema taasisi hiyo imekuwa ikiunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha changamoto zinazowakabili watoto wa kike zinatatuliwa na haki zao zinalindwa.

Alisema licha ya utekelezaji wa waraka unaoruhusu wanafunzi kurejea shuleni, bado wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo unyanyapaa.

Takwimu za Wizara ya Elimu zinaonesha kuwa wasichana 58 walirejea katika mfumo wa elimu baada ya kuacha shule, huku tafiti za taasisi ya Global Women Institute zikionesha kuwa wasichana milioni 60 duniani wamekumbana na ukatili wa kijinsia. Nchini Tanzania, takribani wasichana milioni 14.6 wanakabiliwa na changamoto zinazowazuia kupata haki ya elimu.

Aidha, alibainisha kuwa msichana mmoja kati ya watatu anaolewa kabla ya kufikisha miaka 18, huku mmoja kati ya wanne pekee akifanikiwa kumaliza elimu ya sekondari.

Pia, baadhi ya wasichana hukosa masomo kwa siku nne hadi tano kila mwezi kutokana na changamoto za hedhi.

Chikoti alisema kupitia mradi wa “Rudi Shule”, taasisi hiyo imefanikiwa kuwafikia zaidi ya wasichana 500, na inalenga kuwafikia wanafunzi 250 zaidi mwaka huu, huku ikibainisha kuwa unyanyapaa bado ni kikwazo kikubwa kwa wanafunzi wanaorejea shuleni.

Mmoja wa wanufaika wa kampeni hiyo, Theresa Juma (21), alisema alipata ujauzito akiwa na umri wa miaka 18 baada ya kumaliza kidato cha kwanza hali iliyomlazimu kuacha shule.

Alisema alifukuzwa nyumbani na kupitia changamoto nyingi, lakini aliamua kurejea shuleni huku akijitegemea kugharamia masomo yake.

“Nilifaulu kwa daraja la kwanza, lakini ujauzito ulinikatisha masomo.

Nimepitia changamoto nyingi, lakini nimeamua kujitafutia maisha na kuendelea na elimu yangu huku nikilea mtoto wangu,” alisema Theresa.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...