Na Said Mwishehe, Michuzi TV


MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile, amesema matukio ya waandishi wa habari kukamatwa, kupigwa na kubughudhiwa yamepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na hali ilivyokuwa huko nyuma.

Balile amesema hayo leo Aprili 16, 2026 wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu Maalumu wa jukwaa hilo uliofanyika kwa lengo la kujadili mapendekezo ya marekebisho ya Katiba.

Akizungumzia hali ya vyombo vya habari nchini na mataifa mengine, Balile amesema kumetokea mambo mengi yakiwemo waandishi kupoteza maisha, vyombo vya habari kufungwa na kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.

“Mataifa mbalimbali duniani tumeshuhudia mambo mengi yakitokea katika miaka ya karibuni kwenye tasnia yetu ya habari.

“Waandishi 140 wamepoteza maisha kutokana na vita zinazoendelea kwa baadhi ya nchini, lakini tumeshuhudia katika vyombo vya wenzetu wamepata mtanzuko mkubwa na sasa hivi Sauti ya Amerika (VOA) haipo hewani na chaneli zake zote.

“Pia katika nchi za jirani kuna waaandishi wamezuiliwa kuingia katika nchi. Kwa Tanzania matukio ya waandishi wa habari kukamatwa, kupigwa imepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na zamani.

“Nimekuwa Rais wa Jukwaa la Wahariri la Afrika Mashariki kwa muda mrefu, na nchi ambazo ni wanachama wa jukwaa hilo wanakiri Tanzania iko vizuri, lakini ni wajibu wetu sasa kuzingatia misingi ya taaluma ya habari," amesema.

Akieleza zaidi Balile amesema kuna baadhi ya waandishi wa habari wamekuwa wakiogopa kuandika kabla ya kuzuiliwa kwa maana ya kujizuia kuandika kabla ya kuzuiwa, hivyo ametoa rai ya kuondoa woga huo huku akisisitiza kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi ya taaluma.


UCHUMI WA VYOMBO VYA HABARI

Kuhusu hali ya uchumi katika vyombo vya habari amesema umekumbwa na changamoto kubwa katika mataifa mbalimbali akitolea mfano nchini Marekani ambako magazeti 3,200 yamefungwa na kuondoka sokoni.

Pia, magazeti yaliyokuwa yakipata faida ya mamilioni ya fedha sasa yanajiendesha kwa faida ndogo akitolea mfano kampuni ya Standard nchini Kenya.

“Kwa Tanzania kampuni kama New Habari iliweka historia kwa kujiondoa yenyewe sokoni. Takwimu sio nzuri sana kwa kuwa mapato yamepungua sio katika vyombo vya habari pekee, lakini hadi katika taasisi za habari na sisi Jukwaa la Habari tumekuwa na changamoto za kiuchumi na ndio maana hatujakutana kwa muda mrefu,” amesema.

Kutokana na hali hiyo ametoa rai kwa vyombo vya habari nchini kutafuta vyanzo vipya vya mapato badala ya kutegemea vilivyopo hasusan matangazo na mabaki ya magazeti.

Pamoja na hayo, kwa kipekee ametoa shukrani za dhati kwa niaba ya jukwaa hilo kwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kutokana na kuendelea kuliunga mkono jukwaa la Wahariri.

“Kwa kipekee tunaishukuru WCF kwa kuendelea kutuamini siku hadi siku na wamekuwa wakituwezesha kwa kiwango kikubwa kwa mfano kama walianza kutuchangia kwa sh. milioni tano wakaongeza milioni 10, milioni 15, hadi Sh. milioni 30. Kwa hiyo kwa kipekee tunaishukuru WCF kwa kuendelea kuwa nasi wakati wote.” amesisitiza.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...