Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), kupitia Mkurugenzi Mkuu wake, Ephraim Mafuru, imepokea ugeni maalum kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Abel Makubi, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kukuza utalii wa matibabu nchini Tanzania na kushiriki katika Maadhimisho ya Miaka 10, tarehe 15 July 2026 ambapo pia Hospitali itakuwa ianzindua mfuko wa kusaidia huduma za Upandikizaji Uloto kwa Watoto na Upandikizaji Figo. 

Katika kikao hicho, taasisi hizo mbili zimejadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano na kukubaliana kuendelea kuhamasisha utalii wa Matibabu kama moja ya mazao ya kipekee ya utalii nchini. Hatua hiyo inakuja wakati Hospitali ya Benjamin Mkapa ikiendelea kujipambanua kwa kutoa huduma za kibingwa na ubobezi wa hali ya juu, na kuifanya kuwa miongoni mwa hospitali bora za rufaa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumza katika kikao hicho, Mafuru amesema Bodi ya Utalii imevutiwa sana na huduma sita za kibingwa zinazotolewa na hospitali hiyo, huku huduma mbili zikiwa za kipekee zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Ni jambo la kujivunia Hospitali ya Benjamin Mkapa kuwa hospitali pekee Afrika Mashariki na Kati yenye utaalamu wa kupandikiza uloto kwa watoto waliozaliwa na selimundu (Sickle Cell), lakini pia huduma ya upandikizaji figo,” amesema Mafuru.

Ameeleza kuwa upekee wa hospitali hiyo unaweza kuinua taswira nzuri ya Tanzania katika sekta ya utalii wa tiba, sambamba na kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuwapatia huduma za kibingwa ndani ya nchi badala ya kusafiri nje kutafuta matibabu.

Mafuru pia ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya utalii nchini kushiriki harambee ya kuanzisha mfuko maalum wa kusaidia matibabu ya wagonjwa wa selimundu na figo kwa wananchi wasio na uwezo. Harambee hiyo inatarajiwa kufanyika Julai 15, 2026, sambamba na maadhimisho ya miaka kumi tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Kwa upande wake, Prof. Makubi ameahidi kushirikiana kikamilifu na Bodi ya Utalii Tanzania katika kukuza zao hili la utalii wa tiba nchini, akisisitiza kuwa taasisi zote mbili zipo chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema kuimarishwa kwa utalii wa tiba kutaiwezesha Tanzania kujijengea nafasi kubwa zaidi kama kitovu cha huduma za afya za kibingwa katika ukanda wa Afrika, huku pia ikichangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Ushirikiano huu unaendelea kufungua ukurasa mpya wa kuitangaza Tanzania si tu kama kivutio cha wanyamapori, fukwe na urithi wa utamaduni, bali pia kama kitovu cha huduma za afya za ubora wa kimataifa.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...