Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) leo imezindua rasmi Kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu”, ikiwa ni hatua muhimu katika kuhamasisha usimamizi bora na uadilifu katika sekta ya ushirika nchini. Kampeni hii inalenga kuelimisha na kuhamasisha Wanaushirika na wadau mbalimbali kuhusu umuhimu wa ushirika wenye uadilifu, uwazi, na ufanisi katika kuleta maendeleo endelevu.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika jijini Dodoma, ambapo Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, alikuwemo kama mgeni rasmi kwenye Mkutano wa Wadau wa Maendeleo ya Ushirika. Katika hotuba yake, Chongolo alisisitiza kuwa ushirika ni nguzo muhimu katika uchumi wa Taifa, akiongeza kuwa ushirika wa kiuchumi na kijamii unaweza kutoa suluhu kwa changamoto kubwa zinazokumba sekta ya kilimo na uchumi wa nchi.
"Leo tunazindua kampeni hii kwa lengo la kuweka misingi imara ya ushirika. Ushirika unahitaji uadilifu, uwazi, na usimamizi bora ili uweze kutoa matokeo chanya kwa Wanaushirika na jamii kwa ujumla," alisema Mhe. Chongolo. Aliendelea kusema kuwa sekta ya ushirika ina mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania na kwamba juhudi zote za kuimarisha ushirika ni muhimu katika kuhakikisha nchi inapata maendeleo ya kudumu.
Amesema kuwa, ili sekta ya ushirika iweze kuleta matokeo bora, kila mdau katika sekta hiyo anahitaji kujitolea kwa dhati katika kusimamia rasilimali za ushirika, kwa kuzingatia misingi ya uadilifu na uwazi. "Tunahitaji kuwekeza katika mafunzo, uongozi bora, na kuhakikisha kuwa vyombo vya ushirika vinakuwa na uwezo wa kuongoza na kusimamia kwa ufanisi rasilimali zao," alisema Waziri Chongolo.
Chongolo pia amesisitiza kuwa serikali itaendelea kutoa msaada kwa sekta ya ushirika, ikiwa ni pamoja na kuboresha sera, mikopo, na mifumo ya usimamizi wa mali za ushirika. "Tunapokuwa na ushirika imara, tutakuwa na uchumi imara. Na kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kufikia malengo yetu ya maendeleo endelevu na kuwa na taifa lenye ustawi wa kiuchumi," alieleza.
Kwa upande wake, Dkt. Benson Ndiege, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, amewahimiza Wanaushirika kuwa na ushirika imara na wenye uadilifu ili kuweza kuchangia kwa ufanisi katika uchumi wa Tanzania. Alieleza kuwa ushirika imara ni msingi wa ustawi wa kiuchumi na kijamii katika taifa letu.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta ya ushirika, ikiwa ni pamoja na taasisi za kifedha, vyama vikuu vya ushirika, wakaguzi wa nje, wizara za serikali, na mashirika ya kimataifa, ambao wamejizatiti kutoa mchango wao katika kuimarisha sekta ya ushirika na kuboresha hali ya maisha ya Wanaushirika.
Kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu” ni mwendelezo wa jitihada za TCDC katika kuboresha ufanisi wa ushirika na kuhimiza utawala bora. TCDC inajivunia kufanya kazi kwa karibu na serikali, vyama vya ushirika, na wadau wengine muhimu katika sekta hii kwa lengo la kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii. Kampeni hii pia itahusisha semina, mafunzo, na mikutano ya kujenga uwezo kwa Wanaushirika kote nchini, ili kuhakikisha kuwa ushirika unakuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.




.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...