Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

Serikali imeweka wazi mwelekeo wake wa maendeleo kwa kusisitiza kuwa Mpango na Bajeti ya mwaka 2026/2027 ni hatua ya mwanzo katika utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/2027–2030/2031), unaolenga kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Waziri Mkuu Dkt MWIGULU Nchemba ameyabainisha hayo leo Bungeni Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya mapito na mwelekeo wa kazi za Serikali, Makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2026/27 ambapo amesema kuwa utekelezaji wa Dira 2050 unakusudia kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa thamani ya dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, huku wastani wa pato la mtu mmoja mmoja ukitarajiwa kufikia dola 7,000 kwa mwaka.

Amesisitiza kuwa Dira 2050 ndiyo dira kuu ya maendeleo ya Taifa, hivyo mafanikio yake yanategemea ushiriki wa wadau wote. Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa Serikali, taasisi za dini, sekta binafsi, asasi za kiraia pamoja na wadau wa maendeleo kuhakikisha mipango yao inaendana na vipaumbele vya Dira hiyo. Aidha, aliielekeza Tume ya Mipango kuendelea kutoa elimu kwa umma ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake.

Katika hatua nyingine, Serikali imeendelea kuimarisha uchumi unaoongozwa na sekta binafsi. Katika mwaka 2025/2026, jumla ya miradi 927 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 11.08 ilisajiliwa, hali inayoashiria kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji na kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wa kilimo, Serikali imefanikiwa kuimarisha uzalishaji wa chakula na kuhakikisha usalama wa chakula nchini. Taarifa zinaonesha kuwa tani 23,783,128 za mazao zilizalishwa katika msimu wa 2024/2025, kiwango kinachozidi mahitaji ya tani 18,279,054 kwa mwaka 2025/2026, hivyo kuifanya nchi kuwa na uhakika wa chakula kwa asilimia 130.

Ongezeko hilo limetokana na upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, hususan mbolea inayotolewa kwa ruzuku. Katika msimu wa kilimo wa 2025/2026, Serikali imetoa tani 1,098,990 za mbolea, sawa na asilimia 73.26 ya lengo. Kati ya hizo, tani 574,664.99 zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.03 zimesambazwa kwa wakulima zaidi ya 526,000 kupitia mpango wa ruzuku, hatua iliyochochea matumizi ya pembejeo na kuongeza tija ya uzalishaji.

Kwa ujumla, Serikali inaonesha dhamira ya dhati ya kuijenga Tanzania yenye uchumi imara, unaojitegemea na unaotoa fursa kwa wananchi wake wote kupitia utekelezaji madhubuti wa Dira 2050.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...