Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo,akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2026/27 leo Aprili 9,2026 bungeni jijini Dodoma.
...
Mbunge wa Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, amedhamiria kuwasilisha hoja binafsi bungeni itakayolenga kuishauri Serikali kuanzisha mpango maalum wa mikataba ya ajira za muda mfupi kwa vijana ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.
Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2026/27 bungeni, Jafo alisema mpango huo unaweza kuwa na mfumo wa Ajira za muda (part time employment) utakaodumu kwa kipindi cha miaka mitatu mitatu hadi ifikapo mwaka 2050 ambapo vijana watapata ajira za mikataba na kujipatia uzoefu wa kazi.
Alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi kubwa za kuongeza fursa za ajira kwa vijana tangu aingie madarakani, akisema serikali imefanya kazi kubwa katika kuwawezesha wananchi, lakini bado kuna haja ya kuja na mikakati mipya ya kukabiliana na wimbi la vijana wasio na ajira.
Jafo alibainisha kuwa changamoto ya ajira bado ni kubwa, huku akitoa mfano wa vijana wengi waliopo kwenye shughuli zisizo rasmi kama bodaboda, baadhi yao wakiwa na elimu ya juu ikiwemo stashahada, shahada na kuendelea. Alipendekeza mpango maalum utakaolenga wahitimu hao ili kuwapa nafasi ya kupata ajira za muda na mikataba ya miaka mitatu.
Kwa mujibu wa mapendekezo yake, kila mwaka vijana 50,000 wanaweza kuingizwa kwenye mpango huo, ambapo asilimia 20 wawe wahitimu wa stashahada na asilimia 80 wawe wahitimu wa shahada na kuendelea. Aidha, alipendekeza malipo ya kujikimu ya Shilingi 500,000 kwa wenye stashahada na Shilingi 700,000 kwa wahitimu wa shahada.
Alisema gharama ya utekelezaji wa mpango huo inakadiriwa kufikia Shilingi bilioni 396, huku akisisitiza kuwa mpango huo utasaidia kukuza ujuzi wa vijana, kuongeza uzoefu wa kazi na kupunguza tatizo la ajira nchini.
Pia alipendekeza asilimia 10 zitoke katika mapato ya ndani ya kila Halmashauri, 10 ya gawio la Serikali kutoka kwenye mashirika ya umma, na fedha zingine zitokane na kubana maeneo mengine ya matumizi ya kawaida ya serikali(Recurrent Expenditure) ili zitumike kufadhili mpango huo. Aidha, alishauri mpango huo usimamie kupitia serikali za mitaa na Taasisi za Umma ili kurahisisha upatikanaji wa ajira katika halmashauri mbalimbali na Taasisi hizo za Umma.
Jafo alisisitiza kuwa mpango huo, kama utapitishwa, utaisaidia Serikali kuongeza wigo wa ajira na kuwawezesha vijana wengi zaidi kunufaika na fursa za kiuchumi nchini.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...