Na Pamela Mollel,Arusha .
Katika kuendeleza misingi ya uongozi na ushirikiano wa kikanda, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imefanya makabidhiano ya nafasi ya Katibu Mkuu, ambapo Veronica Nduva amekabidhi madaraka kwa mrithi wake Stephen Patrick Mbundi katika hafla iliyofanyika kwenye makao makuu ya jumuiya hiyo jijini Arusha.
Makabidhiano hayo yamehitimisha rasmi kipindi cha uongozi wa Nduva, aliyeliongoza taasisi hiyo kwa msisitizo wa kuimarisha mshikamano wa nchi wanachama na kusukuma mbele ajenda za maendeleo ya kikanda, hususan katika nyanja za uchumi na ushirikiano wa kimkakati.
Katika kipindi chake cha uongozi, hatua mbalimbali zimechukuliwa katika kuimarisha utekelezaji wa miradi ya pamoja, kukuza biashara ndani ya ukanda na kuweka mazingira rafiki ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Aidha, ameweka msisitizo mkubwa katika umuhimu wa kuendelezwa kwa mshikamano miongoni mwa nchi wanachama, akieleza kuwa mafanikio yaliyofikiwa yanahitaji kulindwa na kuendelezwa kupitia ushirikiano wa karibu wa wadau wote wa maendeleo ndani ya EAC.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu mpya Balozi Mbundi ameanza majukumu yake kwa kueleza dhamira ya kuharakisha utekelezaji wa ajenda kuu za jumuiya, akitaja vipaumbele vya kuimarisha soko la pamoja, kukuza biashara ya ndani ya ukanda na kuongeza ufanisi wa taasisi zake.
Ameeleza kuwa atahakikisha kunakuwepo usimamizi thabiti wa rasilimali, uwajibikaji na uwazi katika utekelezaji wa majukumu ya jumuiya, huku akihimiza ushirikiano wa karibu kati ya nchi wanachama katika kukabiliana na changamoto zilizopo.
Mabadiliko hayo ya uongozi yanakuja katika kipindi ambacho EAC inaendelea kupanuka na kuimarisha nafasi yake kikanda na kimataifa, hali inayoweka matarajio makubwa kwa uongozi mpya katika kusukuma mbele ajenda ya ujumuishaji wa kikanda na ustawi wa wananchi wake.



.jpeg)


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...