Na: Calvin Gwabara – Morogoro.

Wakulima wa kilimo cha mpunga kinachotegemea mvua nchini wamewashukuru watafiti wa Mradi wa Mpunga Himilivu kwa Mabadiliko ya Tabianchi na Rafiki kwa Mazingira barani Afrika (CERA) kwa jitihada walizozianzisha kuzalisha mbegu bora ya mpunga unaohimili changamoto za hali ya hewa ili kuinua kipato cha wakulima wa zao hilo Afrika.

Mtafiti mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt. Atugonza Bilaro akifafanua jambo kwa wakulima wakati wa zoezi hilo Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.

Hayo yamebainishwa na wakulima kutoka mikoa ya Morogoro, Shinyanga na Songwe wakati wa zoezi la ukusanyaji wa takwimu za awali na taarifa mbalimbali muhimu zitakazosaidia watafiti hao kuweza kujua changamoto wanazokabiliana nazo katika kilimo hicho ili kuweza kusaidia wao kuzalisha mbegu mpya zilizoboreshwa ambazo zitaweza kuhimili mabadiliko hayo ya tabia nchi.

Ukusanyaji huo wa takwimu umefanyika kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), katika vijiji nane ukishirikisha wakulima wapatao 258.

Akizungumza na watafiti hao mkulima Bwana Maroja Shana kutoka Kijiji cha Silela kata ya Shilela Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mkoani Shinyanga amesema kuwa ujio wa mradi huo ni ukombozi kwa wakulima wengi wa mpunga nchini ambao wanalima kwa kutegemea mvua na hasa kwenye wilaya yao ambayo zao kubwa la bishara na chakula ni mpunga.

“Zamani tulikuwa tunategemea mvua za msimu ambazo zilikuwa zinanyesha kwa utaratibu unaotabirika, lakini sasa hali imebadilika kabisa maana mvua zinachelewa kuanza au zinanyesha kwa vipindi vifupi sana na kusababisha maji kukosekana mashambani. Hali hii imeathiri sana uzalishaji wangu wa mpunga kwa sababu zao hili linahitaji maji ya kutosha ili likue vizuri. Mara nyingi hulazimika kupanda mara kadhaa bila mafanikio, jambo linaloniongezea gharama na kunipunguzia kipato” alieleza Bwana Shana.

Aliongeza “kutokana na ukame huu wa mara kwa mara, maisha yangu na familia yangu yamekuwa magumu zaidi kwani mavuno yanapopungua, hata chakula cha nyumbani kinakuwa hakitoshi, na wakati mwingine nalazimika kununua chakula ambacho ningepaswa kukizalisha mwenyewe. Pia nashindwa kumudu gharama za pembejeo bora kama mbegu na mbolea, jambo linaloendelea kudidimiza uzalishaji wangu na hali hii inanifanya nitafakari njia mbadala za kilimo, lakini bado nahitaji msaada wa kitaalamu na mbegu bora ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuendelea kujikimu kupitia kilimo cha mpunga”.

Kwa upande wake Zilpa Simchimba, mkulima mwanamke wa mpunga kutoka Wilaya ya Momba Mkoani Songwe amesema kuwa mvua zimekuwa hazitabiriki. Wakati mwingine hazinyeshi kabisa au zinanyesha kwa muda mfupi usiotosha kukua kwa mpunga hali ambayo husababisha mashamba kukauka mapema na kuathiri ukuaji wa zao hilo linalotegemewa sana na familia yake kwa chakula na kipato.

“Nikiwa kama mama, changamoto hizi zinaniumiza zaidi kwa sababu nabeba jukumu la kuhakikisha familia inapata milo ya kila siku na ninapopata mavuno kidogo hulazimika kugawanya chakula kwa uangalifu au wakati mwingine kupunguza idadi ya milo kwa siku ili kukidhi mahitaji ya watoto wangu. Pia huwa nalazimika kuuza sehemu ya mazao kidogo ninayopata ili kukidhi mahitaji mengine muhimu kama ada za shule na huduma za afya, jambo linalozidi kupunguza akiba ya chakula nyumbani” alieleza Zilpa.

Aliongeza “ninaamini kuwa jitihada hizi za watafiti za kutafiti na kuzalisha mbegu za mpunga zinazoweza kuhimili ukame na mabadiliko ya tabia nchi, zinaweza kubadilisha maisha yetu na ya wakulima wengine wanawake, lakini nasisitiza pia tupewe elimu sahihi ya kupambana na changamoto hii wakati tukisubiria kazi hii kubwa waliyoianza watafiti wa mradi huu wa CERA”.

Akizungumza na wakulima wa Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wakati wa zoezi la ukusanyaji wa taarifa za awali za utafiti, Mtafiti Mkuu wa Mradi huo wa CERA, Prof. Suzan Nchimbi Msolla kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), amesema kuwa mradi huo unalenga kuimarisha ustahimilivu wa zao la mpunga dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, hususan ukame, kwa wakulima wa Tanzania na Kenya.

Mtafiti Mkuu wa Mradi huo wa CERA, Prof. Suzan Nchimbi Msolla kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) akizungumza malengo ya zoezi hilo na Mradi wa CERA kwa wakulima wa Mpunga Afrika.

Prof. Msolla ameeleza kuwa miongoni mwa malengo makuu ni pamoja na kupunguza pengo la kijinsia kwa kuwawezesha zaidi wakulima wanawake, hasa wanaoongoza kaya, kupitia uelewa wa mazingira yao na namna jamii zinavyokabiliana na ukame.

“Mradi huu utajikita pia katika kuendeleza mbegu bora za mpunga zinazoweza kuhimili ukame kwa kuingiza sifa za ustahimilivu kwenye mbegu zinazopendwa na wakulima na zinazokidhi mazingira ya ndani. Sambamba na hilo, watafiti watatekeleza mbinu bora za kilimo katika maeneo yenye ukame, ikiwemo matumizi ya upandaji wa moja kwa moja na kilimo cha mzunguko ili kupunguza matumizi ya maji na uzalishaji wa gesi chafuzi na kujenga uwezo wa taasisi za ndani kupitia mafunzo na uwekezaji katika miundombinu ya utafiti” Alifafanua Prof. Msolla.

Kwa mujibu wa Prof. Msolla, matokeo yanayotarajiwa ni pamoja na kuimarika kwa usalama wa chakula na kupungua kwa athari za ukame kwa wakulima, hasa kupitia matumizi ya mbegu zinazostahimili ukame na mbinu bora za kilimo.

Aidha amesema mradi huo utachangia kuongeza uzalishaji na kipato kwa wakulima, huku ukipunguza matumizi ya maji na kulinda mazingira. Pia, mradi utaimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika utafiti wa mpunga na kusaidia taasisi za ndani kuwa na uwezo endelevu wa kufanya tafiti na kuzalisha teknolojia zitakazowanufaisha wakulima kwa muda mrefu.

Mradi huu unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mpunga (IRRI), Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO), na Chuo Kikuu cha Copenhagen kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Denmark (DANIDA).

MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA ZOEZI HILO LA UKUSANYAJI WA TAKWIMU

Mtafiti Mkuu Msaidizi wa mradi huo Dkt. Emanuel Malisa akizungumza na wakulima kuhusu zoezi hilo la ukusanyaji wa takwimu linavyofanyika.

Wakulima wa kilimo cha mpunga kinachotegemea Mvua wakifuatilia maelezo ya watafiti kabla ya kuanza zoezi la udodosaji.

Mtafiti kutoka SUA Bi. Rehema Mollel akizungumza na mkulima wa mpunga kwenye kijiji cha Madoto Wilayani Kilosa.

Mtafiti Mkuu wa Mradi wa CERA, Prof. Suzan Nchimbi Msolla, Mtafiti kutoka TARI Dkt. Atugonza Bilaro na Mtafiti Mkuu Msaidizi wa mradi huo Dkt. Emanuel Malisa wakiwa kwenye majadiliano na wakulima kupata taarifa.




 

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...