Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imezindua rasmi utekelezaji wa mpango wa ufadhili wa masomo ya ufundi kwa vijana nchini unaofahamika kama “NBC Wajibika Scholarship”. Mpango huu ni sehemu ya juhudi endelevu za taasisi hizo mbili katika kuunga mkono azma ya serikali ya kukuza ajira, hasa kwa vijana, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Uzinduzi huo umefanyika katika Makao Makuu ya NBC jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka pande zote mbili, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Sabi alisema kuwa katika hatua ya awali, NBC imetenga jumla ya shilingi milioni 150 kufadhili wanafunzi 588 watakaopatiwa mafunzo ya muda mfupi katika fani mbalimbali za ufundi. Fani hizo ni pamoja na umeme, uhandisi mitambo, ujenzi, pamoja na huduma za hoteli na utalii—sekta ambazo zina mchango mkubwa katika ajira na uchumi wa nchi.

Alifafanua kuwa mafunzo hayo yatadumu kati ya miezi mitatu hadi sita na yatatolewa katika vyuo vya VETA vilivyopo Morogoro (Kihonda) na Mwanza. Aidha, kila mwanafunzi atafunguliwa akaunti ya “NBC Kua Nasi” ili kuwaunganisha na mfumo rasmi wa kifedha, sambamba na kuwapatia fursa za kukuza ujuzi wa kibiashara kupitia majukwaa ya NBC Business Club.

“Kupitia mpango huu, hatulengi kuwapatia vijana vyeti pekee, bali tunawaandaa kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa taifa. Tunaamini uwekezaji huu utasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, ambao kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wako chini ya umri wa miaka 35,” alisisitiza Bw. Sabi.

Kwa upande wake, Bw. Kasore aliipongeza NBC kwa hatua hiyo, akieleza kuwa ufadhili huo utachangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha malengo ya VETA ya kutoa mafunzo kwa wanafunzi 120,000 kila mwaka. Alibainisha kuwa hadi sasa taasisi hiyo imefanikiwa kusajili wanafunzi zaidi ya 101,000, hivyo mpango huo unakuja wakati muafaka.

“Hatua hii ya NBC kufadhili wanafunzi 588 ni mchango mkubwa katika safari yetu ya kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata ujuzi wa kujiajiri na kuajirika. Tunatoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huu, kwani uwekezaji katika elimu ya ufundi ni uwekezaji wa moja kwa moja kwa maendeleo ya jamii,” alisema Bw. Kasore.

Aidha, alieleza kuwa uteuzi wa mikoa ya Morogoro na Mwanza kwa awamu ya kwanza umezingatia mahitaji ya wataalamu katika maeneo hayo, huku akibainisha kuwa hatua inayofuata ni utekelezaji kamili wa mpango huo na uwezekano wa kuupanua katika maeneo mengine nchini.

“Kwa ujumla, uzinduzi wa NBC Wajibika Scholarship unaashiria hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na taasisi za umma katika kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, inayoweza kukabiliana na changamoto za soko la ajira na kuchochea maendeleo jumuishi ya taifa.’’ Alihitimisha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (wa pili kulia) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) , Anthony Kasore (wa pili kushoto) wakionesha mfano wa hundi yenye thamani ya Tsh Milioni 150 ikiwa ni thamani ya ufadhili unaotelewa na benki hiyo katika kufadhili utekelezaji wa mpango wa ufadhili wa masomo ya ufundi kwa vijana nchini unaofahamika kama “NBC Wajibika Scholarship”. Hafla ya uzinduzi wa utekelezaji wa mpango huo ilifanyika leo jijini Dar es Salaam ikihusisha maofisa kutoka pande zote mbili. Kushoto ni Mkuu wa Idara yake ya Sekta ya Umma wa NBC Bi Joyce Maruba na Meneja wa Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Bi Anna Nyoni (Kulia)

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kulia) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) , Anthony Kasore (kushoto) wakionesha mfano wa hundi yenye thamani ya Tsh Milioni 150 ikiwa ni thamani ya ufadhili unaotelewa na benki hiyo katika kufadhili utekelezaji wa mpango wa ufadhili wa masomo ya ufundi kwa vijana nchini unaofahamika kama “NBC Wajibika Scholarship”. Hafla ya uzinduzi wa utekelezaji wa mpango huo ilifanyika leo jijini Dar es Salaam ikihusisha maofisa kutoka pande zote mbili. Katikati ni Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa NBC, Godwin Semunyu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Sabi alisema kuwa katika hatua ya awali, NBC imetenga jumla ya shilingi milioni 150 kufadhili wanafunzi 588 watakaopatiwa mafunzo ya muda mfupi katika fani mbalimbali za ufundi. Fani hizo ni pamoja na umeme, uhandisi mitambo, ujenzi, pamoja na huduma za hoteli na utalii—sekta ambazo zina mchango mkubwa katika ajira na uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Bw. Kasore aliipongeza NBC kwa hatua hiyo, akieleza kuwa ufadhili huo utachangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha malengo ya VETA ya kutoa mafunzo kwa wanafunzi 120,000 kila mwaka. Alibainisha kuwa hadi sasa taasisi hiyo imefanikiwa kusajili wanafunzi zaidi ya 101,000, hivyo mpango huo unakuja wakati muafaka.

Uzinduzi huo umefanyika katika Makao Makuu ya NBC jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka pande zote mbili, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...