Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana na kampuni ya Visa Inc. imezindua kadi mpya ya malipo kwa biashara ikiwa na lengo la kuimarisha udhibiti wa fedha kwa wafanyabiashara kubwa na ndogo, hatua inayohusisha kutenganisha matumizi ya kifedha ya biashara na yale binafsi sambamba na kuongeza uwajibikaji.

Kadi hiyo inayotambulishwa kwa mara ya kwanza nchini, inafahamika kama ‘‘NBC Twiga Platinum Business Debit Visa Card’’ ilizinduliwa jana jioni katika hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, The Kilimanjaro katika hafla iliyohudhuriwa na maofisa na viongozi wa benki wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Theobald Sabi, wafanyabiashara pamoja na maafisa kutoka Visa Inc. wakiongozwa na Makamu Rais na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo ya miamala ya Visa Afrika Mashariki, Chad Pollock.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alisema ujio wa bidhaa hiyo unalenga moja kwa moja kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya biashara, hususan kuchanganya fedha za kampuni na matumizi binafsi.

“Hii si uzinduzi wa kadi tu, bali ni kuwapa wafanyabiashara udhibiti kamili wa fedha zao,” alisema. “Kadri miamala inavyoongezeka na kuwa changamani zaidi, ndivyo umuhimu wa mifumo ya uwazi, nidhamu na uwajibikaji unavyoongezeka.”

Kwa mujibu wa Sabi, kadi hiyo itawawezesha wafanyabiashara kutenganisha wazi matumizi ya fedha za biashara, hatua inayotarajiwa kurahisisha utunzaji wa kumbukumbu za kifedha, kuimarisha usimamizi wa ndani, na kupunguza mianya ya upotevu wa fedha—changamoto zinazoathiri kwa kiasi kikubwa biashara ndogo na za kati (SMEs).

Suluhisho hilo linakuja wakati ambapo biashara nyingi nchini zinaendelea kupanuka na kuvuka mipaka, hali inayoongeza hitaji la mifumo ya malipo iliyo salama, ya haraka na inayokubalika kimataifa. “Kupitia ushirikiano wetu huu na wenzetu wa Visa, kadi hii itawawezesha wafanyabiashara kufanya miamala popote duniani huku wakidhibiti matumizi yao kwa ufanisi.’’ aliongeza

Kwa upande wake, Pollock wa Visa alieleza kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi pana za kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali na kusaidia ukuaji wa biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, akisisitiza umuhimu wa miamala salama na inayofuatilika katika mazingira ya biashara ya kisasa.

Akifafanua zaidi kuhusu faida za kadi hiyo, Meneja Biashara ya Kadi wa NBC, Esnat Hollela alisema ikiwa imeunganishwa moja kwa moja na akaunti ya kampuni, kadi hiyo hutoa huduma ya upatikanaji wa fedha kwa wakati halisi, hivyo kurahisisha usimamizi wa malipo pamoja na kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za kifedha na maandalizi ya taarifa za hesabu na ukaguzi.

“Zaidi ya hayo, kadi hii inakubalika kimataifa kupitia mtandao wa Visa, ikiwa na viwango vya juu vya usalama na njia mbalimbali za malipo, jambo linaloongeza ufanisi wa biashara huku likipunguza utegemezi wa miamala ya fedha taslimu,” alisema.

Aliongeza kuwa, mbali na huduma za kifedha, wamiliki wa kadi hiyo pia watanufaika na huduma za kijamii ikiwemo bima, msamaha wa dhima ya kadi, huduma za rufaa za matibabu, kisheria na huduma za viwanja vya ndege.

“Zaidi watumiaji wa kadi hizi watanufaika na punguzo maalum katika huduma mbalimbali kama usafiri, malazi, ununuzi wa nafasi za ofisi, ununuzi wa matangazo ya kidijitali, data na nyinginezo—hii ikiifanya kuwa suluhisho jumuishi linalosaidia shughuli za biashara pamoja na mahitaji ya kila siku.’’ aliongeza

Wachambuzi wa sekta ya fedha wanaona hatua hii ya NBC kwa kiasi kikubwa itasaida kuleta nidhamu na urasmi zaidi katika usimamizi wa fedha za biashara, hasa kwa wajasiriamali ambao mara nyingi hukumbwa na changamoto za mifumo dhaifu ya kifedha.

Akizungumzia hatua hiyo, mmoja wa wateja wa benki hiyo na mwenye uzoefu na huduma za miamala kidigitali, Mhandisi Henry Kulaya alisisitiza kuwa mkakati wa benki hiyo umekuja wakati muafaka kwa kuwa unalenga kusaidia ukuaji wa biashara kupitia suluhisho za kifedha zenye tija, akieleza kuwa udhibiti mzuri wa matumizi una mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi wa uendeshaji.

“Biashara haiwezi kukua kwa ufanisi bila kuwa na mifumo imara ya usimamizi wa fedha. Kadi hii itatusaidia sana wateja hasa wafanyabiashara kutatua changamoto hiyo moja kwa moja. Ni wazi kwamba kadi hii mpya itakuwa nyenzo muhimu kwa wafanyabiashara kubwa na ndogo kuboresha ufanisi wa shughuli zao kwa kuhakikisha kila muamala unaonekana, unadhibitiwa, na unaendana na malengo ya kampuni’’ alisema.






Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kulia) sambamba na Makamu Rais na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo ya miamala ya Visa Afrika Mashariki, Chad Pollock (kushoto) wakitambulisha muonekano wa kadi mpya ya malipo kwa biashara inayofahamika kama ‘‘NBC Twiga Platinum Business Debit Visa Card’’ ikiwa ni muendelezo za wadau hao kurahisisha miamala na kuimarisha udhibiti wa fedha kwa wafanyabiashara kubwa na ndogo nchini. Kadi ili inayotambulishwa nchini kwa mara ya kwanzania ilizinduliwa jana jioni katika hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, The Kilimanjaro katika hafla iliyohudhuriwa na maofisa na viongozi wa benki hiyo wafanyabiashara pamoja na maafisa kutoka Visa Inc.




Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (wanne kulia) sambamba na Makamu Rais na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo ya miamala ya Visa Afrika Mashariki, Chad Pollock (wa tano kushoto) pamoja na wadau wengine wakitambulisha muonekano wa kadi mpya ya malipo kwa biashara inayofahamika kama ‘‘NBC Twiga Platinum Business Debit Visa Card’’ ikiwa ni muendelezo za wadau hao kurahisisha miamala na kuimarisha udhibiti wa fedha kwa wafanyabiashara kubwa na ndogo nchini. Kadi ili inayotambulishwa nchini kwa mara ya kwanzania ilizinduliwa jana jioni katika hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, The Kilimanjaro katika hafla iliyohudhuriwa na maofisa na viongozi wa benki hiyo wafanyabiashara pamoja na maafisa kutoka Visa Inc.






Kwa upande wake, Makamu Rais na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo ya miamala ya Visa Afrika Mashariki, Chad Pollock (pichani) alieleza kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi pana za kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali na kusaidia ukuaji wa biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, akisisitiza umuhimu wa miamala salama na inayofuatilika katika mazingira ya biashara ya kisasa.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi (pichani) alisema ujio wa bidhaa hiyo unalenga moja kwa moja kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya biashara, hususan kuchanganya fedha za kampuni na matumizi binafsi.


Akifafanua zaidi kuhusu faida za kadi hiyo, Meneja Biashara ya Kadi wa NBC, Esnat Hollela (alieshika kipaza sauti) alisema ikiwa imeunganishwa moja kwa moja na akaunti ya kampuni, kadi hiyo hutoa huduma ya upatikanaji wa fedha kwa wakati halisi, hivyo kurahisisha usimamizi wa malipo pamoja na kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za kifedha na maandalizi ya taarifa za hesabu na ukaguzi.




Viongozi mbalimbali wa Benki ya NBC na Visa Inc, wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi huo.


Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa Benki ya NBC Bw Godwin Semunyu akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi.





Baadhi ya maofisa kutoka Benki ya NBC pamoja na Visa Inc, wakionesha sifa mbalimbali zinazoambatana na kadi hiyo ya ‘‘NBC Twiga Platinum Business Debit Visa Card’’


Hafla hiyo ilipambwa na burudani za aina mbalimbali.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...