Na Karama Kenyunko Michuzi Tv.

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, amesema watu milioni 20 duniani hufariki kila mwaka kutokana na magonjwa ya moyo, huku matumizi ya tumbaku yakitajwa kuwa miongoni mwa visababishi vikuu.

Dkt. Kisenge, ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, amesema hayo leo Aprili Mosi, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa Uzinduzi wa ripoti inayoonesha namna kampuni za Tambuku nchini zinavyoingilia sera za nchi.

“Kama mnavyofahamu, duniani kote magonjwa ya moyo yanachangia vifo vingi, na kati ya watu milioni 20 wanaopoteza maisha kila mwaka, moja ya visababishi vikuu ni matumizi ya tumbaku au uvutaji wa sigara, ukifuatiwa na shinikizo la damu na kisukari,” amesema.

Amesema matatizo yanayotokana na matumizi ya tumbaku, hasa kwa nchi za Afrika, yameongezeka kwa kasi.

Amesema, nchini Tanzania, uvutaji wa sigara na shisha umeongezeka, hali inayoiweka nchi katika alama nyekundu kutokana na kasi hiyo.

Ameonya kuwa kuvuta shisha mpigo nmoj ni hatari zaidi,kwani ni sawa na kuvuta sigara 100 kwa wakati mmoja, jambo linalosababisha madhara makubwa kwenye mishipa ya damu ya moyo.

“Uvutaji huu husababisha mgando wa damu kwenye mishipa ya moyo, ambao unaweza kusababisha kifo cha ghafla au kiharusi. Pia sigara huathiri mapafu na kusababisha saratani, hivyo hushambulia karibu kila kiungo cha mwili,” amesema.

Ameongeza kuwa JKCI imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya sigara na kufungua matawi katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuwafikia wananchi wengi zaidi.

“Katika mikoa 33 tuliyotembelea, tumekutana na wagonjwa wengi, na kwa kiasi kikubwa chanzo kilikuwa ni matumizi ya sigara,” amesema.

Dkt. Kisenge amesema wagonjwa wengi wameathirika kwa kupata matatizo ya moyo, presha na wengine walihitaji vipimo maalum kutokana na madhara hayo.

Aidha ameishauri serikali kuweka mikakati madhubuti, ikiwemo kuongeza kodi kwenye bidhaa za tumbaku na kutunga sheria kali zitakazodhibiti uvutaji wa sigara, hasa katika maeneo ya mikusanyiko ya watu.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kudhibiti Tumbaku nchini(TTCF), Lutgard Kagaruki amesema kuwa utafiti huo unafanyika kila baada ya miaka miwili na imeanza tangu 2019 na kwamba ripoti hii ni ya awamu ya tano .

Ripoti yetu ni sehemu ya ripoti kubwa ya dunia mwaka huu nchi 100 zilishiriki kwenye huu uchunguzi ambapo kwa Afrika nchi 20 ikiwemo nchi yetu zilishiriki.

Amesema kuwa ripoti hiyo inaonesha Tanzania Ina hali mbaya zaidi "kwa bahati mbaya Tanzania tangu mwaka 2019 uchunguzi inaonesha tupo kwenye hali mbaya tupo kwenye mstari mwekundu tunazidi kudidimia wakati wenzetu majirani zetu mfano Kenya, Uganda, Ethiopia, na mataifa mengine Afrika wanafanya vizuri sana"

Ameongeza kuwa utafiti huo umeangalia kanuni ya 5.3 ya mkataba wa kimataifa wa kudhibiti Tumbaku .

"Mkataba huu unazuia kwa nguvu zote kampuni za Tumbaku kuingilia sera za afya,"amesema.

Amesema kuwa matokeo hayo hayaridhishi "ombi letu moja kwa viongozi kwamba tunasheria mbovu iliyotungwa mwaka 2003 kabla mkataba wa Shirika la Afya duniani (WHO), haujaja ambapo ulitoka 2005 kwa hiyo hiyo sheria inamapungufu mengi lakini tulishatengeneza muswada unaoendana na mazingira"

Amesema kuwa muswada huo uliandaliwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo WHO, Wizara ya Afya na wadau wengine "tangu 2017 ulikuwa upelekwe bungeni lakini mpaka leo ujapelekwa na tunaamini ni kwa sababu ya msukumo wa kampuni za Tumbaku,"

"Tunaiomba serikali huu muswada upelekwe bungeni haukatazi kulima Tumbaku au usiuze Tumbaku unaendelea kulinda afya za Watanzania na mazingira yao,"

Amesisitiza kuwa sheria hiyo itasaidia kudhibiti matumizi holela ya tumbaku "watu wasivute hovyo, mmeona shisha ilivyoonea usiwavutishe wengine kwa sababu kwa sasa hivi shisha sote ni wavutaji kama ukikaa pahala kunywa soda, kula chakula, utavuta shisha kwa hiyo tunaiomba serikali ipitishe huo muswada tupate sheria bora itakayoweza kulinda afya za Watanzania,". 

Naye, Daktari wa magonjwa ya ndani na mfumo wa upumuaji, Dkt. Mwanaada Kilima, amesema matumizi ya tumbaku yanaigharimu nchi zaidi kuliko faida inayopatikana.

“Kiasi cha kodi kinachopatikana kutokana na tumbaku ni takribani Sh bilioni 200 kwa mwaka, lakini gharama za matibabu ya madhara yake zinazidi Sh bilioni 800, hivyo ni wazi kuwa si biashara yenye faida bali inaleta hasara kubwa,” amesema.

Ameongeza kuwa mgonjwa mmoja wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji anaweza kutumia zaidi ya Sh milioni nne kwa mwaka kwa matibabu, bila kujumlisha gharama za wagonjwa wa saratani na magonjwa ya moyo.

“Hii inaonesha mzigo mkubwa kwa taifa, na kama hatua hazitachukuliwa, gharama hizi zitaendelea kuongezeka na kuwa changamoto kubwa zaidi,” amesema.

Dkt. Kilima ametoa wito kwa vijana kuacha matumizi ya shisha na sigara, akisisitiza kuwa ni hatari kubwa kwa afya zao.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...