Na Janeth Raphael MichuziTv 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema uzinduzi wa meli ya kwanza ya uvuvi wa bahari kuu ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ni hatua muhimu inayoweka msingi imara wa utekelezaji wa sera na mikakati ya nchi katika kuendeleza sekta ya uvuvi na kukuza uchumi wa buluu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa meli hiyo, Rais Samia alisema hatua hiyo ni sehemu ya mabadiliko ya kimkakati katika usimamizi na udhibiti wa rasilimali za bahari kuu, huku ikilenga kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika uchumi wa taifa.

Rais Samia amesema Serikali imejidhatiti kulifufua na kuliimarisha Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ili liweze kushiriki kikamilifu katika kusimamia na kunufaika na rasilimali zilizopo katika bahari kuu kwa manufaa ya Watanzania wote.

Ameongeza kuwa uzinduzi wa meli hiyo unaakisi maono mapya ya Serikali katika kuhakikisha rasilimali za bahari zinasimamiwa kwa tija, uwazi na ufanisi zaidi, ili kuongeza mapato ya taifa na ajira kwa wananchi.

Katika hotuba yake, Rais Samia pia amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha taasisi nyingine za udhibiti na usimamizi wa rasilimali za uvuvi ili kukabiliana na changamoto ya uvuvi haramu unaoharibu mazingira na kuhatarisha uhai wa viumbe vya majini.

Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kukomesha uvuvi usiozingatia sheria na taratibu, ili kuhakikisha uendelevu wa rasilimali za bahari kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, Rais Samia amesema Serikali imefanya jitihada kubwa kuboresha mazingira ya shughuli za uvuvi katika maziwa na bahari kwa kuwezesha upatikanaji wa mitaji, utaalamu na vifaa, ikiwemo boti za kisasa za uvuvi pamoja na kuendeleza teknolojia za ufugaji samaki kwa njia ya vizimba.

Uzinduzi wa meli hiyo ya kwanza ya uvuvi wa bahari kuu kwa TAFICO unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya uvuvi nchini na kuongeza uwezo wa Tanzania kunufaika na uchumi wa buluu kupitia rasilimali zake za baharini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kuashiria Uzinduzi wa Meli ya Kwanza ya Uvuvi wa Bahari Kuu kwenye hafla fupi iliyofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) Kigamboni Jijini Dar es Salaam tarehe 25 Aprili, 2026.





 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...