Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

Serikali imelenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma, sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi unazingatia ubora unaotakiwa, kwa wakati na kwa thamani halisi ya fedha (Value for Money).

Hayo yameelezwa na Kaimu Kamishina wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma kutoka Wizara ya Fedha, Alex Haraba, wakati akitoa taarifa kwa umma kuelekea uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025.

Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Aprili 8, 2026 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Akizungumzia umuhimu wa sera hiyo, Haraba amesema ni hatua ya kimkakati inayolenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za Serikali kupitia mnyororo wa ugavi.

Amefafanua kuwa sera hiyo inalenga kufungamanisha shughuli zote za mnyororo wa ugavi ili kuimarisha utaratibu na usimamizi jumuishi, kuboresha matumizi ya rasilimali za umma, na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Kwa mujibu wa Haraba, kwa muda mrefu shughuli za mnyororo wa ugavi zimekuwa zikitekelezwa kupitia sheria, kanuni na mifumo mbalimbali bila kuwepo kwa mwongozo mmoja wa kisera unaounganisha hatua zote kwa mtazamo jumuishi.

Amesisitiza kuwa kutokana na sehemu kubwa ya matumizi ya Serikali kupita katika ununuzi wa umma, mnyororo wa ugavi ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha rasilimali za umma zinasimamiwa kwa uwazi, ufanisi na uwajibikaji, hali itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha, sera hiyo inaweka mkazo katika kuimarisha utawala bora, matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa mnyororo wa ugavi, pamoja na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na makundi maalum ya kijamii. Hatua hii inalenga kupanua fursa za kiuchumi na ajira kwa Watanzania, pamoja na kuhamasisha matumizi ya rasilimali na malighafi za ndani ili kuongeza thamani katika uzalishaji wa bidhaa na huduma.

Haraba ameongeza kuwa sera hiyo imeandaliwa kuweka mfumo jumuishi wa kimkakati wa kusimamia shughuli zote za mnyororo wa ugavi katika sekta ya umma. Mfumo huo unahusisha hatua mbalimbali kuanzia upangaji wa mahitaji, ununuzi wa umma, ugomboaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali, upokeaji na ukaguzi wa bidhaa, uhifadhi, matumizi na usambazaji, hadi uondoshaji wa mali za umma.

Uzinduzi wa sera hiyo unatarajiwa kuwa chachu ya maboresho makubwa katika usimamizi wa rasilimali za umma na kuongeza tija katika utoaji wa huduma za Serikali.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...