Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imeweka mkazo katika kuimarisha usalama wa mifumo ya TEHAMA, kuongeza ufanisi wa huduma za kidijitali pamoja na kuunganisha mifumo ya taasisi za umma ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza Bungeni jijini Dodoma Aprili 17, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani J. Kikwete, alisema hatua hizo ni sehemu ya mpango wa maboresho ya huduma za serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Waziri Kikwete alieleza kuwa katika kipindi hicho, e-GA itafanya tathmini ya usalama wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA katika taasisi 571 za umma ili kuhakikisha mifumo hiyo inafanya kazi kwa ufanisi, uimara na usalama wa hali ya juu.

Aidha, Serikali inalenga kuboresha na kuunganisha mifumo jumuishi ya TEHAMA pamoja na mifumo ya kisekta na ya kitaasisi, lengo likiwa ni kupunguza urudufu wa mifumo na kuongeza ushirikiano kati ya taasisi za serikali.

Katika hatua nyingine, e-GA itahusika katika kuchambua, kubuni na kuendeleza mifumo mipya ya kisekta kwa taasisi mbalimbali, ili kurahisisha utoaji huduma na kuongeza ufanisi wa kiutendaji ndani ya serikali.

Serikali pia imepanga kuunganisha taasisi zote za umma kupitia Mfumo wa Kubadilishana Taarifa Serikalini (GovESB), hatua itakayorahisisha mawasiliano na ushirikiano wa kidijitali kati ya taasisi.

Vilevile, juhudi zitaelekezwa katika kuimarisha tafiti na ubunifu wa teknolojia mpya za TEHAMA ili kuibua huduma bora zaidi kwa wananchi, sambamba na kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia zinazoendelea kujitokeza duniani.

Katika kuboresha upatikanaji wa huduma, mtandao wa mawasiliano wa Serikali utapanuliwa hadi kufikia wilaya zote nchini, huku mifumo kama e-Office na huduma nyingine za kidijitali ikiendelea kuboreshwa.

Kwa upande wa miundombinu, e-GA itaendelea kusimamia vituo vya kuhifadhi data za Serikali pamoja na mifumo ya ulinzi dhidi ya majanga ya kimtandao ili kuhakikisha taarifa za serikali zinalindwa wakati wote.

Aidha, Serikali itatoa mafunzo kwa watumishi wa umma na watumiaji wa mifumo ya TEHAMA ili kuongeza uelewa na ufanisi katika matumizi ya teknolojia katika utumishi wa umma.

Kwa ujumla, maboresho hayo yanalenga kuimarisha utawala bora wa kidijitali, kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...