Na, Mwandishi Wetu
Ujumbe wa Serikali ya Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi, imekutana na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola na Rais wa zamani wa Malawi, Mhe. Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera, na kujadiliana kuhusu namna Tanzania ilivyojidhatiti katika kudumisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Kikao hicho kilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) siku ya Alhamisi Aprili 9, 2026 mchana baada ya Mheshimiwa Chakwera kumtembelea Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahamoud Thabit Kombo, ikiwa ni ishara ya kuanza rasmi kwa ziara ya Mjumbe huyo Maalum nchini Tanzania.
Katika kikao hicho, Mhe. Profesa Kabudi alimueleza kwa kina Mjumbe huyo Maalum, kuhusu hatua mbalimbali zinazoendelea kuchululiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuimarisha demokrasia nchini huku ikiweka msisitizo katika kulinda na kuheshimu utu wa Mtanzania, kuzingatia haki na uwajibikaji, amani na utulivu pamoja na kudumisha umoja wa kitaifa.
“Tumekutana na Mheshimiwa Chakwera na tumemueleza mambo mengi kuhusu Tanzania na historia ya nchi hii tangu ipate uhuru mwaka 1961, hali ya siasa na demokrasia nchni, na hatua ambazo serikali inaendelea kuchukua ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa tulivu na kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi jumuishi na kujiletea maendeleo”, ameeleza Waziri Kabudi.
Waziri kabudi ameeleza kuwa kikao hicho kimekuwa kizuri na chenye mafanikio kutokana na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kupata ufafanuzi wa kutosha juu ya masuala mbalimbali yanayoendelea nchini hususani katika kudumisha amani, umoja wa kitaifa na ustawi wa Watanzania.
Mbali na kukutana na ujumbe wa Serikali, Mheshimiwa Chakwera anatarajiwa kukutana na wadau mbalimbali ambapo jana Aprili 10, 2026 alikutana na Msajili wa Vyama vya Siasa, Mhe. Jaji Mstaafu Francis Mutungi pamoja na vyama vya siasa vya ACT–Wazalendo, Chama cha National League for Democracy (NLD), United Democratic Party (UDP), Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Chama cha NCCR Mageuzi, Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Alliance for African Farmers Party (AAFP) na Chama cha ADA-TADEA.
Vyama vingine ni pamoja na Democratic Party (DP), Tanzania Labour Party (TLP), Union for Multiparty Democracy (UMD), United People’s Democratic Party (UPDP), Chama cha Kijamii (CCK), Demokrasia Makini, Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Katika ziara yake hii, Mheshimiwa Chakwera anatarajia pia kukutana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na baada ya Uchaguzi Mkuu, Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Othman Chande, Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jaji Joseph Warioba, Jumuiya zisizo za Kiserikali, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Mhe. Jaji George Joseph Kazi, Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo Mhe. Othman Masoud Othman, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jaji George Mcheche Masaju, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Mhe. Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro.
Aidha, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, atakutana pia na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...